The House of Favourite Newspapers

Yanga, Coastal Union Watamba …Lazima Tuwanyooshe

0

YANGA imekuwa ikipata tabu zaidi ndani ya Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ambapo leo itacheza hapo dhidi ya wenyeji wao, Coastal Union.

 

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wenye pointi 49, wanaingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na rekodi bora ya kutopoteza mechi msimu huu ndani ya ligi hiyo ikicheza mechi 21 sawa na Coastal Union iliyokusanya pointi 23.

 

Yanga inayofundishwa na Kocha Mrundi, Cedric Kaze, ina kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi ya mzunguko wa kwanza kwa mabao 3-0 dhidi ya Coastal pale Uwanja wa Mkapa, Dar.

Rekodi zinaonesha kuwa, tangu msimu wa 2011/12, Yanga imeenda Mkwakwani kupambana na Coastal Union mara saba na kuambulia ushindi mechi mbili, ikipoteza mbili na sare tatu.

Msimu bora kwao ulikuwa 2014/2015 ambapo Yanga ilishinda mechi zote za nyumbani na ugenini. Ugenini ilishinda 1-0 na nyumbani 8-0.

 

Tangu hapo hadi sasa, Yanga ikienda Mkwakwani, haijawahi kuibuka na ushindi ambapo safari hii wanaenda wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichotokea msimu wa 2015/2016.

 

Katika msimu huo, Yanga ilienda kupambana na Coastal ikiwa haijapoteza mechi hata moja kwenye ligi, ikaondoka kwa kuchapwa mabao 2-0.

 

Mechi ya kwanza nyumbani nayo ilishinda 2-0.Sasa kuelekea mchezo huo wa leo, kila upande unatamba kwamba utamnyoosha mwenzake ambapo Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda, amesema: “Tumejipanga vizuri kukabiliana na Yanga na kuzichukua alama zote tatu na kuacha heshima nyumbani.“Tunataka kuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga msimu huu.

 

”YACOUBA AMPA MZUKA KAZE

Yanga ambayo itaikosa huduma ya Carlos Carlinhos ambaye ana adhabu ya kadi nyekundu akitakiwa kukosa mechi tatu kuanzia hii ya leo, imepata nafuu kutokana na kurejea kwa mshambuliaji, Yacouba Songne.

 

Kaze amefunguka kuwa, anaamini kurejea kwa baadhi ya nyota wake muhimu waliokuwa na majeraha akiwemo Yacouba, itawapa nguvu.

 

“Kwanza siwezi kusema kama tulikuwa tunapata wakati mgumu kusaka matokeo, bali ni changamoto za kiufundi na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wetu muhimu.“

 

Lakini jambo zuri ni kwamba tayari baadhi ya nyota hao muhimu ikiwemo Yacouba wamerejea, hali hii inanipa matumaini makubwa ya kuamini tutafanya vizuri katika michezo yetu ijayo.“Tunataka kuanza na mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Coastala Union, ambao ni lazima tushinde ili kuendelea kujiimarisha katika uongozi wa ligi,” alisema Kaze.

STORI: JOEL THOMAS NA CAREEN OSCAR, DAR ES SALAAM

Leave A Reply