The House of Favourite Newspapers

Yanga Hii ya Kibabe Sana

0

YANGA ya msimu ujao itakuwa ni ya kibabe sana. Hivyo ndivyo wanavyotamba mashabiki wa timu hiyo, baada ya kuishuhudia katika tamasha la Siku ya Mwananchi Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam. Tamasha hilo lilihitimishwa na mechi kati ya Yanga na Aigle Noir ya Burundi iliyomalizika kwa ushindi wa Yanga wa bao 2-0.

 

Tamasha hilo, liliamsha mzuka wa mashabiki wa Yanga ambao walianza kuingia uwanjani tangu asubuhi, na ilipofi ka saa nane kamili tayari walikuwa wamefurika uwanjani.

 

Mashabiki wa Yanga jana walijaa uwanjani na kuwafunika wapinzani wao Simba ambao wiki iliyopita walifanya tamasha lao la Simba Day na kuhudhuriwa na mashabiki wengi, lakini si kama ilivyokuwa kwa Yanga jana.

 

Msululu wa mashabiki kuingia uwanjani jana, ulianzia mbali kabisa katika Chuo cha Uhasibu kutokana na wingi wa mashabiki waliotaka kuingia uwanjani. Hadi kufi kia saa nane mchana, mashabiki walikuwa wamejaa robo tatu ya uwanja huku wengine wakiwa nje wakiendelea kuingia. Na kufi kia jioni walikuwa wameshajaa hadi kwenye ngazi.

 

KIKWETE ASHANGILIWA, ATOA NENO ZITO

Tamasha hilo, pia lilihudhuriwa na viongozi wengi wazito akiwemo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye alishangiliwa alipokuwa akitambulishwa.

Alipopewa nafasi ya kuwasalimia Yanga, Kikwete aliwashukuru viongozi na wadhamini wa klabu hiyo huku akimtaja Mkurugenzi wa SportPesa, Tarimba Abbas na kuwakumbusha watu kuwa ni mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni.

Kikwete alisisitiza kuwa ni lazima timu hiyo ihakikishe inapata ubingwa msimu ujao. Aliwashukuru pia wafanyabiashara Rostam Aziz na Ghalib Mohammed kwa kuipenda Yanga na kuisaidia ilipokuwa kwenye shida. Kikwete pia alisisitiza Yanga kufanya uwekezaji kwenye soka la vijana na kudumisha umoja.

 

DULLA MBABE ATUA UWANJANI AKIWA AMEVIMBA JICHO

Bondia maarufu Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’, jana alitinga uwanjani na kukaa sehemu ya wageni maalum huku usoni akiwa bado anaonekana kuvimba juu ya jicho la upande wa kushoto, kutokana na kutoka kupoteza kwenye pambano lake la juzi dhidi ya Twaha Kassim ‘Kiduku”.

 

STEJI NNE

Wakati Simba wao waliandaa steji moja katika tamasha lao la Simba Day, Yanga wenyewe jana walikuwa na steji nne, moja ikiwa eneo la kuingilia huku mbili zikiwa nyuma ya magoli ya uwanja na ya mwisho ikiwa upande wa mashabiki.

 

WACHEZAJI WATINGA NA SUTI

Majira ya saa 10:30, wachezaji wa Yanga waliamsha shangwe baada ya kutinga uwanjani na kuzunguka kuwasalimia mashabiki wakiwa na suti zao nadhifu za rangi ya bluu na raba nyeupe, wakiongozwa na Haruna Niyonzima na Deus Kaseke waliokuwa wameshika bango la kuishukuru SportPesa.

 

BILLNASS, G-NAKO WAPAGAWISHA

Wasanii wa Bongo Fleva, Billnass na G-Nako waliwapagawisha mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo, baada ya kuingia uwanjani wakiwa wamepanda guta na kuzunguka uwanja mzima.

 

HARMONIZE ASHUKA NA KAMBA UWANJANI

Mwanamuziki mahiri wa Bongo Fleva, Harmonize, aliwadatisha mashabiki baada ya kuingia uwanjani kwa kutumia kamba iliyofungwa kutokea upande wa Magharibi mwa uwanja kuelekea mashariki akiwa amevaa mavazi yanayofanana na ya kijeshi.

Ulinzi uliimarishwa uwanjani wakati Harmonize akishuka kwa kamba, kulikuwa na walinzi wake na polisi wa farasi waliozunguka uwanja mzima. Lakini Harmonize alidondoka kwa bahati mbaya alipokuwa anatua mara baada ya wahusika kukosea kumshusha.

Baada ya hapo, Harmo alipiga bonge la shoo akiwa na jumla ya madansa 40 kwenye steji nne, kila steji ikiwa na madansa kumi.

 

WASANII WENGINE

Wasanii wengine waliopanda na kupiga bonge la shoo ni Chegge, Shilole, Baba Levo, G-Nako, Billnass, Juma Nature na Madee.

 

MORRISON ATAMBULISHWA YANGA, MASHABIKI WAMKATAA

Utambulisho wa wachezaji wa Yanga ulianza saa 12:04 baada ya shoo ya Harmonize na Yanga walimtambulisha pia Bernard Morrison kama mchezaji wao wakisema sakata lake lipo kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Kimichezo (Cas). Lakini wakati lilipotajwa jina lake, mashabiki walisikika wakizomea wakisema hawamtaki.

 

UTAMBULISHO WA SENZO WALETA SHANGWE

Feisal Salum ‘Fei Toto’, Tusila Kisinda, Mukoko Tonombe, Carlinhos, Farid Mussa, Mapinduzi Balama, Bakari Mwamnyeto ni baadhi ya wachezaji walioshangiliwa sana wakati wakitambulishwa.

Pia kiongozi mpya wa Yanga, Senzo Mazingisa aliyetokea Simba, naye alishangiliwa vilivyo wakati akitambulishwa uwanjani hapo. Senzo aliichezea timu ya maveterani wa Yanga dhidi ya wachezaji wa zamani iliyomalizika kwa sare ya 2-2. Kocha mpya Zlatko Krmpotic naye alitambulishwa pamoja na msaidizi wake Juma Mwambusi.

 

YANGA VS AIGLE NOIR

Yanga ilianza kucheza saa 1:05 usiku dhidi ya Aigle Noir ya Burundi. Kikosi cha kwanza cha Yanga kiliundwa na Metacha Mnata, Kibwana Shomary/Paul Godfrey dk 68, Yassin Mustapha/Adeyum Saleh dk 68, Abdallah Shaibu ‘Ninja’/Carlinhos dk 82, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe/Zawadi Mauya dk 53, Deus Kaseke/ Juma Mahadhi dk 68, Feisal Salum/Haruna Niyonzima dk 53, Michael Sarpong/ Kiondo adamu dk 68, Ditram Nchimbi/Wazir Junior dk 53 na Tuisila Kisinda/Farid Mussa dk 53.

 

Kisinda alikuwa ni moto wa kuotea mbali katika mchezo huo hadi kuna watu wasikika wakisema huyu ni sawa na Morrison saba.

 

Pia Fei Toto aliwakonga vilivyo mashabiki kwa soka lake safi . Kisinda aliipatia Yanga bao dakika ya 38 akitumia vizuri pasi iliyopigwa na Fei Toto.

 

Bao linguine lilifungwa na Mghana Michael Sarpong kwa kichwa cha kiwango cha kimataifa, akiunganisha pasi safi ya Ditram Nchimbi. Kisinda nusura aipatie Yanga bao la pili dakika ya 45+1, alipopiga shuti kali akiwa nje ya 18, likaokolewa kwa kichwa na beki wa Aigle Noir.

 

Aigle walicheza pungufu kwa muda mrefu wa mchezo huo baada ya mchezaji wao kupewa kadi ya pili ya njano kipindi cha kwanza kabla Yanga hawajapata bao. Kadi hiyo ilisababisha wapoteze ubora wao ambao waliutumia kuikamia Yanga kwa muda mrefu kabla ya kadi hiyo.

 

Beki Shomary Kibwana naye alikuwa moto sana kwenye mchezo huo akionyesha umahiri mkubwa katika kupanda kusaidia mashambulizi. Bakari Mwamnyeto naye alionekana ni imara kwenye eneo la ulinzi huku naye kipindi cha kwanza akipanda kufanya shambulio moja ambalo liliokolewa na kipa.

 

Mustapha Yassin alionyesha uimara mkubwa katika kupiga faulo na pasi fupifupi. Mshambuliaji Sogne Yacouba, anatarajiwa kutua leo Jumatatu akitokea Asante Kotoko. Tayari yupo safarini kuja kuongeza kasi Jangwani. Waandishi: Joel Thomas, Careen Oscar na Marco Mzumbe.

WAANDISHI WETU, Dar es Salaam

Leave A Reply