Yanga Ilala Wagomea Uchaguzi, Wapingwa

Mashabiki wa timu ya Yanga.

WANACHAMA wa Tawi la Yanga – Pluijm Ilala, wameonyesha hali ya kugomea uchaguzi wa klabu hiyo ambao wagombea wake wapo katika hatua ya kupiga kampeni za mwisho kuelekea kwenye hatua ya kupiga kura keshokutwa Jumapili katika Bwalo la Polisi Oysterbay.

 

Kupitia kwa mwenyekiti wa tawi hilo, Said Amanzi ambaye alifika kwenye ofisi za gazeti hili jana Alhamisi, ameeleza kuwa wamelazimika kusambaza barua mbalimbali za maazimio ya wanachama wao wakiupinga uchaguzi huo kwa kile wanachodai hawawezi kushiriki jambo ambalo linakinzana na sheria na kanuni zilizopo kwenye katiba ya klabu hiyo.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Amanzi alisema: “Tunashangazwa sana na waziri mwenye dhamana ya hili kushindwa kuamua jambo dogo kama hili, kiasi kwamba kila kukicha wanakaa vikao ambavyo maamuzi yake yanakuwa ya upande mmoja na ya kusikitisha sana.

 

“Kama waziri aligundua kuna makosa ya kimsingi ilifanya TFF na Yanga iweje hukumu ibaki kwa Yanga kusimamiwa uchaguzi wake wakati kamati yetu ipo wazi na haihusiani na TFF na kwa nini hawa TFF na wao wasingechukuliwa hatua.

 

“Kwa hili ilibidi waziri afanye fair play kama mchezo wa mpira ulivyo, hivyo aamue TFF waombe radhi kwa kuboronga kisha Yanga iachiwe haki yake na ifanye uchaguzi wake kwa kusimamia yenyewe ili mambo yaishe kwa busara hiyo.”

 

Licha ya tamko hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela alinukuliwa akisema wagombea wanatakiwa kufanya kampeni kwa amani bila kumchafua mwingine na mgombea anaruhusiwa kujinadi kokote ikiwemo katika tawi lolote la Yanga.

 

Naye, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia ni Msaidizi wa Kaimu Mwenyekiti, Siza Lyimo aliwataka wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo.

Stori na Musa Mateja,

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment