The House of Favourite Newspapers

Yanga Itawafanyizia USM Algiers, Manji Arejea Kwa Kishindo

Wachezaji wa USM Algiers  wakipongezana.

HURUMA ya kugawa pointi na kung’ang’ania mkiani mwa kundi D la Kombe la Shirikisho kumeifanya Yanga iwe timu ya kwanza Afrika kuondolewa kwenye mashindano hayo msimu huu.

 

Lakini Kocha Mwinyi Zahera ametamka kwamba leo Jumapili watawapiga USM Algiers kwenye Uwanja wa Taifa kulinda heshima ya klabu na taarifa mpya ni kwamba Mwenyekiti wao aliyejiuzulu, Yusuf Manji ataibuka kuangalia mechi.

 

Yanga ambayo itacheza saa 1 usiku imewaambia mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii kwamba Manji ataibuka baada ya kukosekana uwanjani kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wao aliyejiuzulu, Yusuf Manji ataibuka kuangalia mechi.

Tofauti na matarajio ya mashabiki kwamba Yanga ingezikung’uta timu zenye uzito wake ambazo ni Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sports ya nchini Rwanda, Yanga imejikuta kwenye hali mbaya tangu mashindano hayo yaanze ikiwa imeambulia pointi moja tu katika mechi nne.

 

 

Mchezo wa leo huenda ukawa sehemu ya mazoezi mazuri ya ligi kwa Yanga kutokana na maingizo ya sura kadhaa mpya ambazo hazikucheza mechi za awali za mashindano hayo kutokana usajili kuchelewa.

 

Uwepo wa Mkongomani Herietier Makambo na kurejea kwa Amissi Tambwe kwa upande wa ushambuliaji unaongeza nguvu zaidi kwenye safu hiyo ambayo tegemeo lao alikuwa Matheo Antony ambaye hana uzoefu.

 

Kwenye ulinzi, ameingia beki mzoefu, Kelvin Yondani ambaye atasaidiana na mabeki wenzake Juma Abdul na Andrew Vicent huku langoni akianza kwa mara ya kwanza kimataifa, kipa Mkongo, Klaus Kindoki.

Deus Kaseke ambaye kwenye mchezo uliopita dhidi ya Gormahia alifanya kazi kubwa, leo atasaidia kusukuma mashambulizi.

 

“Tunaendelea vizuri na maandalizi yetu ya kujiandaa na ligi kuu lakini pia mechi ya USM Alger. Hali ya kikosi changu kusema kweli ni nzuri na ninavutiwa zaidi na hali ya kujituma uwanjani inayoonyeshwa kila siku na wachezaji wangu,” alisema Zahera ambaye ana uraia wa DR Congo na Ufaransa.

Comments are closed.