Yanga Jeuri, Yashusha Waarabu Wawili

YANGA ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mipango ya kuwaleta makocha wawili kutoka nchini Tunisia ambao ni kocha msaidizi na wa viungo. Hiyo ni katika kuelekea msimu ujao ili kuhakikisha wanafanya vema katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

 

Yanga hivi karibuni ilitangaza kuachana na kocha wake msaidizi Jawab Sabri na yule wa viungo, Fareed Casssiem, ambao mikataba yao imemalizika.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, makocha hao watatua nchini mara baada ya timu hiyo itaporejea ikitokea nchini Morocco ambako wameweka kambi.

 

Mtoa taarifa huyo alisema hivi sasa wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kuwaleta mara baada ya kumalizana nao. Aliongeza kuwa makocha hao watakaowaleta ni chaguo na kocha mkuu wa timu hiyo, Mtunisia Nasreddine Nabi.

 

“Tupo huku Morocco bila ya kocha msaidizi na viungo, lakini mara baada ya kurejea nyumbani makocha hao watakuwa tayari wamejiunga na timu. “Hivi sasa tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kuwaleta nchini tayari kwa kuanza kazi ya  kuifundisha Yanga.

 

“Makocha hao watakuja nchini kufundisha Yanga baada ya kupitishwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu ambao ni chaguo la kocha Nabi ambao anaamini akifanya nao kazi watafanya kwa ufanisi mzuri,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo alisema kuwa “Hivi sasa nipo Zanzibar katika uzinduzi wa Tamasha la Wiki ya Mwananchi, naomba nitafute baadaye.” Alipotafutwa baadaye hakupokea simu.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam


Toa comment