The House of Favourite Newspapers

Yanga Kama Wote Taifa, Kukipiga na Mbao

  

YANGA ambayo imeanza kujiandaa na usajili wa dirisha dogo linalofunguliwa Novemba 15, leo Jumapili itacheza na Mbao kwenye mechi ya Ligi Kuu ambayo hakuna dalili yoyote ya sare wala suluhu.

 

Rekodi za Mbao tangu iingie Ligi Kuu zinaonyesha imecheza na Yanga mara mbili kwenye Uwanja wa Taifa imepoteza mechi zote mbili kwa idadi kubwa ya mabao.

 

Lakini na wenyewe wakiwa CCM Kirumba kwenye Uwanja wao wa nyumbani wameifanyia Yanga hivyohivyo. Timu hizo hazikuwahi kutoka sare wala suluhu, wakikutana huwa ni vipigo tu.

Yanga ambayo mechi iliyopita ilitoka suluhu na Simba, leo itaongozwa na kocha wa viungo Noel Mwandila kwani Mwinyi Zahera yupo kwao DR Congo akiiongoza timu yake ya taifa kuwavaa Zimbabwe kwenye mechi ya kufuzu Afcon.

 

Mbao ambayo ipo chini ya kocha mwenye mapenzi makubwa na Simba, Amri Said, imeongoza msimamo wa ligi mara kadhaa msimu huu na ina pointi 14 ambazo ni nyingi zaidi ya Yanga yenye 13.

 

Mbao licha ya kusajili kwa bajeti ya kawaida imeonyesha mabadiliko makubwa msimu huu kwani katika mechi zake nae, imeshinda nne, sare mbili na kupoteza mbili.

 

Katika hatua nyingine,habari kutoka ndani ya Yanga zinasema vigogo wa timu hiyo wameanza kujiweka sawa na dirisha dogo la usajili linaloanza Novemba 15 na kumalizika Desemba 15. Habari zinasema mchakato huo wameuanza mapema kutokana na udhaifu waliouona kwenye safu ya ulinzi na kiungo na tayari kocha Zahera ana majina mfukoni.

STORI NA MWANDISHI WETU

Comments are closed.