The House of Favourite Newspapers

Yanga Kuivaa Coastal Kibabe leo

0


KIKOSI cha Yanga leo kinatarajiwa kujitupa uwanjani kuvaana na Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Bara huku kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi akimtaka kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza kuhakikisha anapambana ili apate namba ya kudumu.

 

Kauli hiyo aliitoa kocha huyo wakati timu hiyo ikijiandaa na mchezo wake wa ligi dhidi ya Coastal utakaopigwa saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Yanga ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 10 sawa na Simba ya pili inayopishana kwa idadi ya mabao ya kufunga huku Azam FC wakiongoza katika msimamo wa ligi wakiwa na 12.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwambusi alisema kuwa, wana matarajio makubwa ya kupata pointi tatu kutokana na maandalizi waliyoyafanya ikiwemo kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM ya Unguja, Zanzibar.

 

Mwambusi alisema kuwa, hivi sasa wanatengeneza kikosi cha ushindani kwa kuhakikisha mchezaji anapambana ili kupata nafasi ya kucheza kwa kuanzia mchezo wa leo dhidi ya Coastal.“Kama benchi la ufundi bado tunaendelea kukisuka kikosi chetu na kikubwa kuona timu inapata matokeo mazuri ya ushindi ili tupate pointi tatu na hilo linawezekana kwetu kutokana na maandalizi tuliyoyafanya.

 

“Hivi sasa tumejaribu kutengeneza ushindani wa namba katika kikosi chetu, hiyo ndiyo sababu ya kucheza mechi nyingi za kirafiki na kikubwa ni kupata kikosi cha kwanza kitakachocheza kwa kuelewana, hivyo tumemtaka kila mchezaji atakayepata nafasi ya kupambana ili aingie katika kikosi cha kwanza kwa kuanzia mechi hii ya ligi dhidi ya Coastal, ”alisema Mwambusi.

Naye Kocha Mkuu wa Coastal, Juma Mgunda alisema kuwa walianza vibaya michezo minne iliyopita baada ya kuondokewa wachezaji wao muhimu na kwa sasa anajaribu kukiboresha kikosi chake kwa kuanzia safu ya golikipa, mabeki, viungo na washambuliaji.

 

“Mashabiki wetu wa Coastal nawaomba waendelee kutupa sapoti kwenye mechi zetu zinazofuatia ikiwemo dhidi ya Yanga, tunafahamu wanahitaji ushindi na burudani kutoka kwenye timu yao.

 

“Timu yetu ina wachezaji wengi vijana na wapya ambao wanaendelea kuzoeana na nina imani tutafanya vizuri huko mbeleni ukiwemo mchezo wetu unaofuatia dhidi ya Yanga, tunawaheshimu wapinzani wetu lakini tunaahidi kupambana.”

Leave A Reply