The House of Favourite Newspapers

Yanga Kushusha Vifaa Vinne

0

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umepanga kutumia kipindi hiki cha kusimamishwa kwa Ligi Kuu Bara kama mwanya wa kufanya usajili wa wachezaji wanne raia wa kigeni kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu hiyo.

 

Kwa sasa Yanga inaonekana kukata tamaa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya wapinzani wao, Simba, kuwaacha kwa tofauti ya pointi 20 licha ya kuwachapa katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo, Machi 8, mwaka huu.

 

Taarifa ambazo Championi Ijumaa imezipata kuhusiana na masuala ya usajili ndani ya klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao ni kwamba, uongozi wa Yanga umepanga kukamilisha usajili wa wachezaji wanne raia wa kigeni ndani ya kipindi hiki ambacho ligi imesimamishwa kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona.

 

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo amesema kuwa, wamepanga kukamilisha usajili wa wachezaji wanne raia wa kigeni ambao watachukua nafasi za wachezaji wengine wa kigeni ambao wataachwa mwishoni mwa msimu huu, hiyo ni kutokana na kuonyesha viwango vya kawaida, lakini wachezaji hao wanatarajiwa kuja kusaini mikataba na kisha kuondoka huku wakitarajiwa kurejea kipindi cha maandalizi ya msimu ujao.

“Kwa sasa tunafanya shughuli nyingine ndani ya timu, lakini kuhusu usajili tumepanga kuleta wachezaji wanne wa kigeni ambao watakuja kusaini mikataba na kuondoka kurejea nchini kwao na watarudi kujiunga na timu rasmi wakati wa timu itakapokuwa inafanya maandalizi ya msimu ujao,” alisema kiongozi huyo.

 

Licha ya Yanga kuonekana wakianza harakati za usajili mapema, huenda mchakato huo unaonekana kuwa mgumu kukamilika kutokana na mlipuko wa Virusi vya Corona ambapo kwa sasa vinawalazimu wageni wote kutoka nje ya nchi ya Tanzania kukaa Karantini kwa muda wa siku 14 wakati wanapoingia nchini, jambo ambalo litawalazimu Yanga kuingia gharama kuwahudumia wachezaji hao watakapokuwa Karantini.

 

Hakukuwa na kiongozi wa Yanga aliyepatikana kulifafanua jambo hilo hadi gazeti hili lilipokuwa likiingia mtamboni.

Leave A Reply