Kartra

Yanga Mbaroni Tuhuma Za Mauaji

Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, linamshikilia Yanga Sesa,mkazi wa Mwanishai Meatu mkoani Simiyu kwa mahojiano kufuatia mauaji ya Machiya Mayunga, (45),mkazi wa Kijiji cha Chikola wilaya ya Manyoni ambaye aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na watu wasiofahamika.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida ACP Stella Mutabihirwa, imeeleza chanzo cha mauaji hayo inasadikika ni mgogoro wa kifamilia uliotokana na kugombania ng’ombe wapatao 80 aliopewa marehemu na Baba yake mzazi kwa ajili ya kuwatunza.

 

Tukio hilo limetokea Oktoba 11, 2021, majira ya saa 5:00 usiku, ambapo imeelezwa kwamba mtuhumiwa walimvizia marehemu akiwa nje ya nyumba yake akila chakula na ndipo walimshambulia kwa fimbo kisha kumkata na shoka aliyokuwa akitumia marehemu kujihami baada ya kudondoshwa chini.

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linaendelea na msako mkali kuwasaka watuhumiwa waliohusika katika mauaji hayo ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.


Toa comment