The House of Favourite Newspapers

Yanga Mkubali Dante Awe ‘Mbuzi’

0

HADITHI ya beki wa kati wa Yanga , Vicent Andrew maarufu kama Dante imechukua sura mpya baada ya mashitaka kufika kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Dante amefungua mashitaka yake akiidai Yanga kitita cha Sh milioni 40 ikiwa ni sehemu ya malipo yake kadhaa, zikiwemo fedha za usajili.

 

Wakati Dante anadai, tayari alichukua uamuzi wa kususia kuichezea Yanga hadi pale atakapolipwa fedha zake hizo ambazo amezidai kwa zaidi ya msimu mmoja na nusu bila ya mafanikio.

 

Uongozi wa Yanga kupitia msemaji wake, Hassan Bumbuli umeeleza ulikuwa tayari kumlipa Dante na ulikubaliana naye kwamba ungeendelea kumlipa kidogokidogo au kwa mafungu.

 

Hata hivyo, Dante akaamua kwenda kushitaki, jambo ambalo wanaona kama limewashangaza huku wakiwa wanaamini hata TFF nayo ikipitisha alipwe, lazima itakuwa kwa mafungu.

 

Hakuna ubishi kweli Yanga haiko katika hali nzuri sana ya kulipa fedha zote hizo kwa wakati mmoja, hili ni jambo liko wazi na tunaamini uongozi wa Yanga utakuwa hauongopi katika hilo.

 

Pia, kitu kingine kizuri kabisa katika sakata hili ni kwamba, uongozi wa Yanga haijakataa kulipa na haujakataa kama unadaiwa. Badala yake unasema upo tayari kulipa taratibu.

 

Pamoja na hivyo, sote tunajua kuwa Dante ameamua kugoma baada ya uvumilivu kumshinda. Kwamba alijitahidi kuvumilia kwa muda mrefu lakini ahadi zimeendelea bila ya kutimizwa na suala la subiri limekuwa kwa muda mrefu sana.

 

Huenda uongozi wa sasa wa Yanga unaweza usiwe unayajua machungu ya Dante kwa asilimia kubwa kwa kuwa wakati akipambanana “njaa” yake, viongozi waliopo sasa hawakuwa wameingia madarakani, hivyo kwanza hawapaswi kulaumiwa kwa yale ya zamani lakini nao wanapaswa kurudi nyuma na kutazama upya alikopitia Dante.

 

Hakuna hata mtu mmoja anayeweza kunyoosha mkono na kusema Dante si beki mzuri, si beki aliyeitumikia Yanga kwa juhudi na maarifa au si mchapakazi.

 

Lakini nani anayeweza kuendelea kuchapa kazi bila ya kuwa na taswira ya ubora wa maisha yake ya kesho wakati ni kijana anayepambana kutengeneza maisha yake ya baadaye.

 

Vizuri tukajikumbusha, wachezaji nao ni binadamu kama sisi na wanapokuwa wanazitumikia timu wanakuwa kazini na wangependa kupata maendeleo kama tupendavyo sisi tunapoamka na kwenda makazini au katika biashara zetu.

 

Hivyo tusiwakandamize kwa kisingizio cha mapenzi. Kikubwa Yanga na Dante, bado wana nafasi ya kukaa mezani na niwakumbushe, si vibaya wakaunda urafiki wa mbuzi na majani.

 

Mmoja mfano Yanga wakubali kuwa majani na Dante au mbuzi au yeye awe mbuzi na wao wawe majani. Mbuzi, anategemea majani kuendesha maisha yake.

 

Lakini baada ya kula, naye anayapa haki kwa kujisaidia na baadaye inakuwa mbolea ya kukuza majani mengine yenye rutuba ambayo yanakuwa msaada kwa maisha ya mbuzi hapo baadaye. Dante anapaswa kulishwa ili aishi Yanga baadaye akiwaameshiba.

 

Ana mahitaji yake kama mwanadamu na kama akitimizwa basi atakuwa faida kubwa au msaada sahihi kwa kikosi cha Yanga. Tukubaliane kuwa mwanadamu yoyote, iwe mimi au wewe, anachoshwa na ahadi zisizotimizika. Kama mtu anakuahidi mara moja, mbili, tatu na akaendelea bila kutimiza, baadaye inaingiza fikra nyingine mfano dharau na kadhalika.

 

Dante amevumilia kwa muda mrefu akiendelea kuitumikia Yanga na bado mambo hayakuwa mazuri. Hivyo alipofikia, amechoka na aeleweke kwamba anastahili chake kwa kuwa ni haki yake. Hivyo, Yanga ianze kuonyesha mfano kwa kumlipa kwanza na si maneno. Inawezekana, kwa kuwa hali ni mbaya lakini haki ni ya Dante, basi alipwe hata robo.

 

Halafu Yanga iweke kauli dhabiti ambayo inaweza kuwa na ushahidi wa TFF kwa kuwa jambo hilo limeshafika huko, mwisho Dante arejee kazini kiroho safi na kuisaidia klabu yake kwa kuwa kuna maisha baada ya deni. Ninaamini usikivu, uvumilivu na busara ya kutosha inaweza kuwa msaada mkubwa wa kulimaliza hili suala ambalo hakika, kukiwa na nia njema, ni jepesi sana.

 

Leave A Reply