NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa afya njema aliyonipatia na ni matumaini yangu upo poa, msomaji wa safu hii.
Joto la Ligi Kuu Bara limeendelea kupamba moto kufuatia michezo mitatu kuchezwa hadi sasa ambapo kumeonyesha kuwa na ushindani mkubwa katika kila mechi.
Kila timu inahitaji kupata matokeo mazuri hasa katika mechi hizi za awali ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya msimamo wa ligi. Hali hiyo inasababisha upinzani kuongezeka zaidi hivyo kufanya kila mechi iwe ngumu.
Hali hii, imeonyesha matokeo tofauti kwa baadhi ya timu ambazo zimekuwa na uhakika wa kuibuka na ushindi katika mechi fulani fulani hali ambayo inaleta changamoto kubwa kutokana na mabadiliko hayo.
Msimu huu ligi inaonekana itakuwa ngumu kutokana na udhamini ambao umeongezeka kwa kasi katika baadhi ya timu shiriki za ligi kuu hali inayowafanya wachezaji kucheza kwa kujituma kutokana na uhakika wa kupata mahitaji yao, hali ambayo italeta upinzani wa hali ya juu.
Kutokana na hali hiyo, hali imeonekana tofauti kwa upande wa Yanga ambayo msimu uliopita ilianza vyema mechi za awali ambapo kipindi kama hiki ilikuwa na pointi saba tofauti na sasa ambapo ina pointi tano.
Hali hiyo imesababishwa kuwe na vuguvugu la kutaka kumtimua kocha George Lwandamina kutokana na matokeo hayo hali ambayo inaleta sintofahamu.
Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya timu hususan timu kubwa kuanza kutimua makocha katika mechi chache pale wanapoona matokeo yanakuwa mabaya hata kama kocha aliwapatia mafanikio katika msimu uliopita.
Klabu na mashabiki wanatakiwa kuwa wavumilivu hasa pale timu zao zinapoteleza kwenye mechi chache kwa kumpa muda kocha aweze kujipanga kwa kutambua tatizo la kikosi chake na kulifanyia kazi.
Ni kweli kocha anaajiriwa huku akiwa yupo tayari kufukuzwa wakati wowote, lakini katika hili Lwandamina anapaswa kupewa muda na si kufanya maamuzi ya haraka ambayo kwa asilimia kubwa yataigharimu timu katika mambo mbalimbali likiwemo suala la fedha.
Kumtolea tathimini kocha ndani ya mechi tatu tu na kufikiria suala la kumtimua si jambo jema kwani litaendelea kuleta madhara zaidi badala ya kujenga kwa kuwa anakuwa ameathiriwa kisaikolojia.
Naamini yeye ni kocha mzuri, na anatambua kile ambacho kinatokea katika timu yake ili kuweza kukifanyia kazi, sidhani hata kama na yeye anafurahia matokeo hayo, jambo la msingi ni vyema akapewa muda wa mechi kadhaa na ikionekana kuwa hali bado ndipo mchakato uweze kufanyika wa hayo mabadiliko, lakini bado nina imani naye ya kuweza kufanya vyema kwa kuwa ni kocha bora.
Kubadilisha kocha katika kipindi hiki ni sawa na kujiingiza shimoni kwa kuwa kocha mpya atakayekuja atakuwa hajui mazingira ya ligi yetu na pia kila kocha huwa na falsafa yake, hivyo itabidi asome mazingira kisha ndiyo aje kukaa sawa.
Mashabiki wanatakiwa wafahamu kuwa, katika mpira kuna matokeo matatu kushinda, kufungwa na kutoa sare, hivyo kinachotokea katika timu ya Yanga ni matokeo ya kawaida na ninaamini kuwa kocha ameona upungufu na ataufanyia kazi.
Kitu kinachowaumiza mashabiki ni kutokana na mazingira waliyojiwekea kichwani kwamba timu yao ni lazima ishinde kila mechi jambo ambalo si sahihi na wanatakiwa kutambua kuwa hata wapinzani wanaokutana nao wanajiandaa na wanahitaji ushindi, hivyo kujihakikishia ushindi wa moja kwa moja ni sawa na kujipa presha.
Nakumbuka katika misimu kadhaa iliyopita, Simba walikuwa wakibadilisha makocha mara kwa mara pale walipoona matokeo yanakuwa mabaya lakini mwisho wa siku timu iliendelea kufanya vibaya zaidi badala ya kufanya vizuri ambapo kulisababaisha kushindwa kuupata ubingwa kwa misimu kadhaa.
NA KHADIJA MNGWAI | ACHA NISEME | CHAMPIONI JUMATANO