Kartra

Yanga Nyodo Tupu, Waipiga Kijembe Simba SC

YANGA ni kama imewapiga kijembe watani wao Simba, ni baada ya kutamka kuwa thamani ya klabu hiyo ni kuanzia Sh 34.8Bil kwa mwekezaji atakayekuja kuwekeza Jangwani.

 

Kauli hiyo huenda ikawa kama kijembe kwa Simba chini ya mwekezaji wao Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye alitangaza kuwekeza klabu hiyo kwa Sh 20Bil.

 

Yanga wanapata jeuri hiyo baada ya juzi kuingia mkataba huo wa Sh 34.8Bil na Azam Media wa kuonyesha mahudhui ya klabu hiyo ikiwemo mazoezi, mechi za kirafiki na mahojiano maalum ya wachezaji na viongozi.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa mwekezaji atakayekuja kuwekeza klabu hapo ni lazima afahamu ukubwa na thamani kabla ya kuja kuwekeza.

 

Bumbuli alisema kikubwa wanataka kuwa mfano kwa klabu za Afrika katika uwekezaji wao baada ya juzi kuweka historia nchini ya mkataba huo mnono wa Sh Bil 34.8.

 

Aliongeza kuwa mara baada ya kukamilika kwa mfumo wa mabadiliko wa klabu hiyo, wakaguzi wa mahesabu watafanya mahesabu ya mali za klabu na baada ya hapo itatajwa thamani ya Yanga ambayo wanaamini itazidi hiyo ya Sh 34.8Bil ambazo wamezipata kutoka Azam Media.

 

“Kiukweli Azam wameonyesha thamani na ukubwa wa Yanga baada ya kuingia mkataba mnono wa kuonyesha mahudhui ya timu yetu ikiwemo mechi za kirafiki na mashindano, mazoezi na mahojiano maalum na wachezaji, kocha.

 

“Ni heshima kubwa waliyotujengea hivi sasa Afrika na duniani kote, hii imeonyesha ukubwa na thamani ya Yanga ambayo hiyo ni salamu kwa mwekezaji atakayekuja kuwekeza kwenye klabu yetu lazima kiwango cha pesa kiongezeke kuzidi hichi ambacho tumekipata kutoka Azam Media.

 

“Yanga ni lazima tuwe tofauti na klabu nyingine na kutaka kuleta utofauti ni lazima thamani yetu iwe kubwa katika uwekezaji katika kuelekea mfumo wa mabadiliko,” alisema Bumbuli.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam


Toa comment