The House of Favourite Newspapers

Yanga sasa imekaa sawa

YANGA imewapa maneno matamu mashabiki wake kwa kusema sasa kikosi chake kimekaa sawa na kipo kamili kuweza kushinda mechi ya leo Jumamosi dhidi ya Lipuli FC.

Yanga inacheza mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara kuanza mzunguko wa pili ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa huku ikiwa imetoka kushinda mechi ya 32 Bora ya Kombe la FA dhidi ya Ihefu FC.

 

Katika mchezo dhidi ya Ihefu, Yanga ilibanwa hadi dakika ya 90 iliposawazisha na kumaliza kwa sare ya bao 1-1 kisha ikashinda kwa penalti 4-3, kiwango cha Yanga siku hiyo hakikuwafurahisha baadhi ya mashabiki wake.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa, kikosi chao kipo sawa hivi sasa na kikubwa wanataka pointi tatu kwa wapinzani wao Lipuli.

Yanga ina pointi 28 katika nafasi ya tatu, imesema inataka kushinda mechi hiyo ili kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Simba na Azam FC zilizo juu yake. Simba ipo kileleni na pointi 35, Azam ya pili ina pointi 30.

Nsajigwa ambaye ni nahodha na beki wa zamani wa Yanga, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika na wataingia uwanjani kwa ajili ya kushinda tu.

 

“Hakuna mechi nyepesi kwetu, kila mechi tunaichukulia kama fainali na kikubwa tunataka kupunguza idadi ya pointi ambazo wapinzani wetu Simba wanaongoza katika ligi.

“Tunashukuru timu imekaa sawa sasa, tupo vizuri na hakuna majeruhi aliyepatikana baada ya mechi na Ihefu, timu itaingia uwanjani kwa lengo moja la ushindi, pia nafurahi morali ya wachezaji ipo juu sana.

“Hatutawadharau wenyeji kwani tulitoka nao sare katika mzunguko wa kwanza, hivyo watapambana kushinda nyumbani ila sisi pia tutapambana kushinda,” alisema Nsajigwa anayemsaidia bosi wake George Lwandamina.

 

Wakati huohuo, Kocha wa Lipuli, Selemani Matola akizungumzia mchezo huo, alisema: “Sisi tumejiandaa vizuri na tumemaliza kazi ya kuwapa mbinu mbalimbali za ushindi wachezaji wetu ili tushinde.

“Tutacheza kwa tahadhari kwani wapinzani wetu wana wachezaji wengi wenye uzoefu wa kimataifa kama Tshishimbi (Papy), Chirwa (Obrey) na Yondani (Kelvin), hawa wanaweza kutupa ugumu.”

Matola ambaye timu yake ipo nafasi ya saba na pointi 16, alisema anafurahia kupona kwa beki wake Joseph Owino aliyekuwa akisumbuliwa na nyama za paja.

 

Wilbert Moland, Dar es Salaam

Comments are closed.