The House of Favourite Newspapers

Yanga SC imekamilika, Mtibwa Sugar kazi wanayo

0

KATIKA kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga wamepata jeuri ya ushindi baada ya kurejea kwa mabeki wake wawili tegemeo.

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana kesho Jumatano saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Manungu uliopo Turiani mkoani Morogoro.

Mchezo huo ni wa mwisho kumalizia mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara. Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Yanga, Haji Manara, alisema upo uwezekano mkubwa wa beki wao Kibwana Shomari kuwepo katika mchezo huo baada ya kupona majeraha yake ya goti.

Manara alisema pia katika mchezo huo atakuwepo beki Djuma Shaban ambaye amemaliza kutumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu. Aliongeza kuwa, mchezo huo ni muhimu kwao kupata ushindi ili waendelee kukaa kileleni katika msimamo wa ligi.

“Maandilizi ya mchezo wetu wa ligi dhidi ya Mtibwa yamekamilika katika kupata ushindi utakaotupa pointi tatu. “Timu inaoondoka leo (jana) mchana kuelekea Morogoro tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao muhimu kushinda.

“Katika msafara wetu atakuwepo Shomari aliyepona majeraha yake ya goti, pia atakuwepo Djuma ambaye adhabu yake ya kusimamishwa michezo mitatu kumalizika, hivyo watakuwa sehemu ya kikosi chetu.

“Katika kuongeza hamasa ya timu yetu viwanjani katika kila mchezo wetu, tumefanya punguzo za jezi zetu katika maduka yetu na sasa bei ya rejareja tunauza 30,000 na jumla 22,000 tu,” alisema Manara.

Katika hatua nyingine, Yanga imetambulisha wimbo wake mpya uitwao Yanga Tamu uliyoimbwa na msanii Omary Ally maarufu Marioo. Akizungumzia hilo, Marioo alisema: “Rasmi nimehamia Yanga nikitokea Simba, huu wimbo nimewatungia Wanayanga ambao watakuwa wakiimba uwanjani.”

WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

Leave A Reply