The House of Favourite Newspapers

Yanga SC Inahitaji Maandalizi ya Kutosha Siyo Kauli Mbiu za Manara

0

KIKOSI cha Yanga kilishuka dimbani Wikiendi iliyopita kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya awali wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United, ambapo Yanga ilikubali kipigo cha bao 1-0.

 

Bila kupepesa macho Yanga hawakuwa na maandalizi bora ya msimu, ni kama hawakuwa tayari kushiriki michuano mikubwa kama hii kutokana na aina ya maandalizi ambayo waliyafanya.

 

Waliweka kambi ya siku tano nchini Morocco, ambayo kwa kiasi kikubwa haikuwa na matokeo chanya kwa upande wao.

Ni kama waliwekeza zaidi nguvu kwenye maandalizi ya Tamasha la Wiki ya Mwananchi, kuliko kuwekeza kwenye maandalizi bora kuelekea msimu mpya wa mashindano kuanzia kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

 

Usajili ambao waliufanya kwa kiasi kikubwa haukuwa na shaka yoyote, wachezaji ambao walisajiliwa wana uwezo mkubwa uwanjani.

 

Usajili mkubwa wa wachezaji bora si suluhisho kwa timu kufanya vizuri kwani wachezaji wanahitaji maandalizi ya kutosha kwenye uwanja wa mazoezi, ili kutengeneza muunganiko ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo cha timu kupata matokeo chanya jambo ambalo kwa Yanga halikufanyika.

 

Kilichowakuta Yanga ni matokeo ya maandalizi mabovu ya msimu ambayo yameleta matokeo ambayo hayaridhishi.

Tumemsikia kocha mkuu wa Yanga, Mohammed Nabi akilalamika kutopata muda wa kutosha kwenye maandalizi kama sababu kubwa kwa kikosi chake kushindwa kupata matokeo.

 

Kuelekea mchezo uliopita Yanga waliwekeza nguvu kubwa kwenye kauli mbiu za msemaji wao, Haji Manara ambaye kwa kiasi kikubwa ziliwaaminisha wana kikosi imara cha kuweza kuwapa matokeo uwanjani.

 

Kauli mbiu siyo suluhisho pekee kwa timu kufanya vizuri, bali ni maandalizi ya kutosha kwenye uwanja wa mazoezi ndiyo yanazipa nguvu kauli mbiu ambazo zinatolewa kuelekea mechi hizi.

 

Kwa kilichotokea kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanaco ni ishara tosha kuwa Yanga ilihitaji maandalizi ya kutosha kuelekea michuano ya kimataifa, hivyo tulitarajia benchi la ufundi lingeyafanyia kazi mapungufu yote ambayo yalijitokeza kwenye mchezo ule.

 

Kwenye mchezo dhidi ya Rivers United Yanga walizidiwa katika kila eneo kuanzianafasi ya ulinzi hadi eneo la ushambuliaji, timu ilionekana kukosa muunganiko tangu kipindi cha kwanza jambo lililosababisha wakaruhusu bao la kawaida ambalo hatukutarajia timu kama Yanga inayonolewa na mmoja ya makocha bora kuruhusu bao la aina ile.

 

Kuelekea Nigeria kwenye mchezo wa marudiano Yanga wanahitaji zaidi kufanya maandalizi ya kutosha kwenye uwanja wa mazoezi na si kwenye kauli mbiu za Haji Manara, kauli mbiu za Manara haziwezi kuwa Muarobaini tosha kwa timu kupata matokeo uwanjani.

 

Benchi la ufundi linapaswa kuyafanyia kazi mapungufu yote ambayo yamejitokeza kwenye mchezo wa kwanza ili yasiweze kujirudia kwenye mchezo wa marudiano.

 

Yanga wana wiki moja ya kufanya maandalizi kabla ya mechi ya jasho na damu kule Port Harcourt, ambayo Yanga wanahitaji ushindi mkubwa ili waweze kufuzu hatua inayofuata.

 

Kwa upande wa wachezaji mnapaswa kutambua kuwa mna deni kubwa kutoka kwa Watanzania, na Wanayanga ambao kiu yao ni kuona timu za Tanzania zinafanya vizuri na kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa.

 

Ni muda wenu kutambua kuwa mna jukumu zito la kuipambania nembo ya Yanga, kwani matarajio makubwa ya mashabiki wenu ni kuona timu inafanya vizuri. Maandalizi yakiwa ya kutosha hata kauli mbiu za Manara zitakuwa na nguvu, lakini maandalizi yakiwa hafifu hakuna shabiki ambaye atajali kauli mbiu za Manara, bali lawama zitarudi kwa wachezaji na benchi la ufundi.

 

Yanga haipaswi kukimbia kivuli chake, jambo pekee wanalopaswa kulifanya kwa sasa ni kuwekeza nguvu kubwa mazoezini na si porojo za mitandaoni ambazo hazina tija kwa klabu. Mchezo wa marudiano ni zaidi ya mechi kwani wapinzani wenu tayari wana faida ya bao la ugenini, hivyo mnapaswa kupambana kwenye dakika zote tisini kwenye mchezo huo.

 

Kama Rivers wameweza kupata matokeo kwa Mkapa, hata Yanga pia wanaweza kupata matokeo kule Port Harcourt kikubwa ni kufanya maandalizi ya kutosha na si kauli mbiu za kutosha.

HUSSEIN MSOLEKA

Leave A Reply