The House of Favourite Newspapers

Yanga SC Wambana Morrison Kwa Saa Tatu

0

YANGA haitaki utani kwani usiku wa kuamkia jana, uongozi wa timu hiyo ulifanya kikao kizito na kiungo wao mshambuliaji, Mghana, Bernard Morrison, kwa zaidi ya saa tatu.

 

Morrison alitua Yanga katika dirisha dogo la usajili msimu huu, ambapo hadi sasa amefanikiwa kuifungia timu hiyo mabao manne huku akionekana ‘kuwashika’ mashabiki wa timu hiyo hasa baada ya kuifunga Simba Machi 8, mwaka huu na mechi kuisha kwa Yanga kushinda bao 1-0.

 

Hivi karibuni kumekuwa na majibizano mengi kuhusiana na Morrison na dhidi ya timu inayommiliki kwa sasa, Yanga kuhusiana na mkataba baina ya pande hizo.

 

Morrison anasema mkataba wake unamalizika baada ya ligi kuisha huku Yanga wakidai walimuongeza miaka miwili hivyo unamalizika Julai, 2022.

Kitendo hiki kimeufanya kila upande uzungumze kwenye vyombo mbalimbali vya habari huku Morrison akitumia Gazeti la Championi kama sehemu sahihi ya yeye kufikisha ujumbe kwa kuwa anajua linafika sehemu kubwa Tanzania, jamaa alitiririka kwelikweli, pia unaweza kumcheki live kupitia Global TV Online.

 

Habari kutoka ndani ya Yanga, zimeweka wazi kuwa, usiku wa kuamkia jana Ijumaa, uongozi wa timu hiyo ulikutana na Morrison kwenye kambi yao iliyopo Regency Hotel, Mikocheni jijini Dar na kumuweka chini kwa zaidi ya saa tatu ikimtaka aweke wazi madai yake ya kusema hajasaini miaka miwili ndani klabu hiyo.

 

“Morrison ameendelea kuonyesha jeuri kubwa sana kwetu, jambo ambalo sasa tumeamua nasi kumuonyesha kuwa hakuna mchezaji mkubwa zaidi ya klabu yetu, hivyo jana (juzi Alhamisi) tuliamua kumuita na kukaa naye ili aseme nia yake nini hadi aamue kutangaza hana mkataba wakati anajua aliongeza miaka miwili.

 

“Suala hili ni kubwa sana kwetu na tunaamini kama Morrison asipobadilika basi ajuwe hao wanaomtuma ili atuvuruge wataishia kumuona tu akiishia benchi maana hatuna jinsi nyingine ya kuendelea kubishana na mtu anayetaka kuipanda kichwani klabu yetu ingawa tunafahamu pia kweli kuna watu wanamshawishi avunje mkataba kinyemela,” kilisema chanzo hicho.

 

Championi lilimtafuta Morrison ili aweze kuzungumzia ishu ya kikao chake na mabosi wake lakini simu yake iliita na haikupokelewa.

 

YATAJA ITAKAOWASAJILI

Naye Mwandishi Khadija Mngwai amezungumza na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela ambapo ametaja aina ya wachezaji ambao watawasajili msimu ujao kwenye timu yao.

 

Mwakalebela amefunguka kuwa, wanahitaji kufanya usajili ulio makini na wa kiwango cha juu msimu ujao ili kuepuka changamoto za hapa na pale kutoka kwa wachezaji na timu kuwa chini ya kiwango.

 

“Kwa sasa mtazamo wetu haupo kwa Morrison, kuna mambo mengi ya kufanya na ya kuyazungumzia katika klabu yetu ya Yanga kuliko kumzungumzia yeye.“Tunajipanga kuhakikisha tunakuwa makini zaidi katika usajili wa msimu ujao wa ligi kuu, tunahitaji kuwa na kikosi kipana kilicho imara na cha ubingwa, kila mchezaji atakayepata nafasi ya kusajiliwa ni lazima awe anapata nafasi katika timu aliyotokea.

 

“Kwa sasa tunajipanga kuhakikisha tunafanikiwa kushinda mechi zote zilizo mbele yetu na ule mchezo wa FA ili kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.”

Leave A Reply