The House of Favourite Newspapers

Yanga waapa kufa na Simba SC

UONGOZI wa Yanga umesema kuwa baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa juzi Jumamosi dhidi ya Azam FC, sasa unajipanga kuhakikisha unatetea ubingwa wake.

Simba ndiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara lakini ushindi wa Yanga juzi dhidi ya wapinzani wengine wa ubingwa, Azam FC, umewapa matumaini ya kuutetea.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, wanajipanga kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mechi zake zote zilizobakia, hivyo timu zote zilizoko mbele yao katika msimamo wa ligi zijipange.

 

“Baada ya kutoka katika michuano ya Mapinduzi hakika timu yetu haikuwa sawa, kiwango ilichokionyesha kiliwaudhi watu wengi lakini kwa sisi viongozi tulijua kuwa wachezaji wengi walikuwa wamechoka kwa sababu michuano hiyo haina afya kwao zaidi ya kuwaumiza.

 

“Kiwango walichoonyesha dhidi ya Mwadui na Ruvu Shooting hakika kilikuwa kibovu lakini dhidi ya Azam kila mtu anasema lake, kwa hiyo kasi hiyo ndiyo tutakayoenda nayo na kocha wetu mkuu George Lwandamina katuambia hivyo.

“Kutokana na hali hiyo, timu zote zilizopo mbele yetu zijiandae kutupisha, matatizo yote waliyokuwa nayo wachezaji tumeshayamaliza, kwa hiyo kilichobaki kwao ni kazi tu na siyo kitu kingine,” alisema Nyika

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam.

Comments are closed.