The House of Favourite Newspapers

Yanga waifuata Mbao kwa pipa

YANGA ni kama imewawekea ubishi watani wao wa jadi, Simba, ni baada ya leo alfajiri kutarajia kusafiri kwa ndege kwenda kuwafuata wapinzani wao Mbao FC ya mkoani Mwanza.

Hiyo, ikiwa ni siku moja kabla ya Simba jana asubuhi kupanda ndege kuwafuata African Lyon huko Arusha. Wakati Simba wakitarajiwa kujitupa uwanjani kesho Jumanne, Yanga wao watavaana na Mbao keshokutwa Jumatano katika michezo ya ligi.

Akizungumza na Championi Jumatatu, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema kuwa timu hiyo inatarajiwa kusafiri kwa Shirika la Ndege la Air Tanzania. Saleh alisema, msafara wa timu hiyo unatarajiwa kuwa na wachezaji 20 na viongozi wote wa Benchi la Ufundi la Yanga linaloongozwa na Mkongoman, Mwinyi Zahera.

“Baada ya mchezo wa jana (juzi), wachezaji waliruhusiwa kwenda kusalimia familia zao na leo Jumapili asubuhi timu iliingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Mbao. “Hivyo, timu inatarajiwa kusafiri kesho (leo Jumatatu) alfajiri kwa ndege kuelekea mkoani Mwanza kwa ajili ya mchezo wetu wa ligi na Mbao tutakaoucheza Jumatano hii,” alisema Saleh.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Comments are closed.