Yanga wamchangia Manara fedha za matibabu

manara

Sweetbert Lukonge,

Dar es Salaam

OFISA Habari wa Simba, Haji Manara, hivi karibuni alipata matatizo ya macho baada ya jicho lake moja kupoteza uwezo wa kuona, wakati akiendelea na matibabu, wanachama wa Yanga wameamua kumchangia fedha za matibabu katika kile walichodai kuonyesha michezo siyo uadui.

Wanachama hao wameongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro ambaye alithibitisha juu ya mchango huo kwa kusema kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na kuguswa zaidi na tatizo hilo ambalo limempata Manara kama ndugu na mdau mkubwa katika soka nchini.

“Soka siyo uadui bali ni mchezo unaotuweka pamoja, pia upinzani wa Simba na Yanga upo uwanjani ila nje ya uwanja sisi sote ni ndugu, tatizo alilopata Manara ni kubwa.

“Kutokana na hali hiyo tukiwa kama wanafamilia wenzake na ndugu zake imetubidi tuchangishane ili kuhakikisha tunapata kiasi fulani cha fedha kitakachomsaidia katika matibabu yake.

“Tumepanga kuwa kama ataenda nje ya nchi basi gharama zote za nauli ya kwenda na kurudi ziwe kutoka kwa wanachama na mashabiki wa Yanga, hata hivyo mpaka sasa tumeshachangishana zaidi ya shilingi milioni moja na bado tunaendelea,” alisema Muro na kuongeza:

“Fedha hizo tutamkabidhi siku yoyote ile kuanzia leo mara tu tutaka-pokutana kwa pamoja na waratibu wa zoezi hili.”

Alipotafutwa Manara ili aweze kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana kufuatia simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa.

Toa comment