Yanga wamfuata Baba Kessy
Beki wa Simba, Hassan Kessy.
Waandishi Wetu, Dar es Salaam
SIKU chache baada ya Yanga kuifunga Simba mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara, imefahamika kuwa ‘figisufigisu’ za usajili zimeanza kunukia na zaidi ni kuhusu beki wa Simba, Hassan Kessy.
Kessy ambaye alicheza dhidi ya Yanga na kufanya kosa ambalo lilizaa bao la kwanza, amejikuta katika wakati mgumu kutokana na kupokea lawama na vitisho vingi kutokana na kosa lake hilo, imeelezwa kuwa anaweza kuwa mali ya Yanga kama kila kitu kitaenda sawa na ikiwa Simba haitamuongezea mkataba mpya kutokana na ule wa sasa kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu.
Katika kile kinachoonekana kweli Yanga wanamhitaji beki huyo, gazeti hili limepata taarifa kuwa kuna wanachama na wadau wa Yanga wa matawi jijini Dar waliamua kumfuata baba mzazi wa mchezaji huyo kwa nia moja ya kumshawishi mwanaye ili akubali kujiunga na Yanga mwishoni mwa msimu huu.
Chanzo kutoka ndani ya Yanga kimesema kuwa, baada ya mechi hiyo, Kessy alinukuliwa na gazeti hili akisema kuwa amepokea vitisho kutokana na kosa alilofanya, hivyo wao kwa kuwa wanaona ni mchezaji mzuri wakaamua kumfuata baba yake ili azungumze na mwanaye amshawishi ajiunge na Yanga pindi ofa itakapopelekwa rasmi.
Gazeti hili lilipomtafuta Kessy hakupatikana kutokana na simu yake kutokuwa hewani muda mwingi.
Alipotafutwa meneja wa Kessy, Athuman Tippo kuhusu madai hayo, alisema: “Hata kama ni kweli wamezungumza na baba yake, jambo la msingi ni kufuata taratibu zinazotakiwa ili wamsajili, sisi tunachoangalia ni dau nono na mazungumzo yatakavyokuwa kwa kuwa mkataba wake unaelekea mwishoni.”
Baada ya mazungumzo hayo ikabainika kuwa Kessy amebadili namba ya simu na haijulikani kwa watu wengi.
Alipotafutwa kwa namba hiyo mpya, Kessy alisema: “Nipo hospitali ninaumwa nimekutwa na malaria tatu, nitakutafuta baadaye.” Alipotafutwa baadaye hakupokea.
Alipotafutwa Daktari wa Simba, Yassin Gembe, simu yake haikupatikana hewani, alipotafutwa Meneja wa Simba, Abbas Ally, alisema mchezaji majeruhi zaidi ya Paul Kiongera ni Haji Ugando kuhusu Kessy alisema: “Haumwi na yupo hapa mazoezini.”