Yanga Wana Nafasi ya Kufuzu Nusu Fainali
Yanga wakifanya mazoezi.
Na Leonard Msigwa
MWAKA 1918 wakati Vita ya Kwanza ya Dunia ikiwa imepamba moto, kiongozi wa Urusi, Vladimir Leninm alitembelea uwanja wa mapambano kuwapa morali wanajeshi wake. Kamanda mmoja akamwambia Lenin, “mkuu ni bora turudishe vikosi nyuma, askari wetu wanazidi kuangamia.” Lenin alimjibu, “askari wa kweli ni yule anayeipigania nchi yake hadi mwisho.” Hatimaye, Jeshi la Urusi lilishinda vita.
Timu ya Yanga inashiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika pamoja na timu za TP Mazembe (DR Congo), Medeama (Ghana) na MO Bejaia (Algeria). Mpaka sasa Yanga imecheza michezo minne na kupoteza michezo mitatu na kutoka sare mchezo mmoja dhidi ya Medeama uliopigwa jijini Dar es Saalam.
Msimamo wa kundi hilo mpaka sasa timu ya TP Mazembe inaongoza kwa kuweka kibindoni pointi kumi ikifuatiwa na Medeama yenye pointi tano ikifungana kwa pointi na Mo Bejaia tofauti yao ikiwa kwenye magoli ya kufunga, huku Yanga ikishika mkia kwa kuwa na pointi moja kibindoni.
Kama kamanda wa kikosi cha Urusi aliyemwomba kiongozi Vladimir Lenin waondoe kikosi vitani kwa kile alichodai askari wengi wanapotea uwanja wa mapambano, ndivyo mashabiki wengi nchini walivyopoteza imani na kukata tamaa na timu yao kwamba tayari imeshaondolewa kwenye nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali.
Zipo sababu nyingi ambazo zinachangia mashabiki wengi kukata tamaa kubwa ni uwezo wa timu yao kuwa dhaifu inapocheza ugenini na namna inavyoshindwa kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani. Ambapo katika michezo miwili ya nyumbani imeambulia pointi moja tu na miwili iliyocheza nje ya nchi kuambulia patupu.
Timu ya Yanga bado ina nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali na wanachotakiwa ni kujipanga zaidi na kuyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza kabla ya kupambana na Mo Bejaia na TP Mazembe.
Kwanza, Yanga inatakiwa kushinda pambano lake dhidi ya timu ya Mo Bejaia litakalopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Saalam. Wakati Yanga ikishinda inatakiwa kuiombea ushindi pia timu ya TP Mazembe itakayocheza na Medeama nchini Ghana.
Pili, Endapo Yanga itashinda pambano lake dhidi ya Mo Bejaia na timu ya TP Mazembe kushinda dhidi ya Medeama basi mtihani utakuwa mwepesi kwa timu ya Yanga ambayo itatakiwa kushinda pambano lake la mwisho dhidi ya TP Mazembe ambao tayari watakuwa wamefuzu hatua ya nusu fainali huku wakiombea timu za Medeama na Mo Bejaia zitoke sare ya aina yoyote.
Endapo matokeo yatakuwa hivyo msimamo wa kundi utakuwa TP Mazembe pointi 13, Yanga pointi 7, Medeama pointi 6 na Mo Bejaia pointi 6. Hivyo timu za Yanga na TP Mazembe zitakuwa zimefuzu hatua ya nusu fainali.
Mchezo wa soka siku zote ni mchezo wa hesabu, na hakuna jambo lolote linaloshindikana kwenye mchezo wa soka.
Siku zote soka huambatana na matukio ya kushangaza, matukio yenye kufurahisha na kuhuzunisha lakini mwisho wa siku maisha yanendelea.
Bado Yanga wana nafasi ya kufuzu, wasikate tamaa bali wajipange na kukubali kukosolewa na kuyafanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza kwenye michezo minne ya awali.
Ni wakati wa benchi la ufundi la timu hiyo kuonyesha kwamba wana uwezo na sifa za kushiriki hatua hiyo ya makundi na hawakupangwa kwa bahati mbaya kama wapinzani wao wanavyosema.
Jukumu lao kubwa ni kuamsha morali ya kupambana na kupigana hadi hatua ya mwisho kama walivyopambana wanajeshi wa Urusi ambao baadaye walishinda vita japo wengi wao walipoteza maisha na wengine kupata vilema vya kudumu. Naamini inawezekana.
Msimamo wa kundi.
NO: | TIMU | MP | W | D | L | G | PTS |
1 | MAZEMBE | 4 | 3 | 1 | 0 | 5:1 | 10 |
2 | MEDEAMA | 4 | 1 | 2 | 1 | 5:5 | 5 |
3 | MO BEJAIA | 4 | 1 | 2 | 1 | 1:1 | 5 |
4 | YANGA | 4 | 0 | 1 | 3 | 2:6 | 1 |