The House of Favourite Newspapers

Yanga Wanatakiwa kuwa Makini na Waarabu

Na MAULID KITENGE |CHAMPIONI IJUMAA| BILA YA KUPEPESA

ALIYEKUWA Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye aliondolewa kwenye nafasi hiyo na sasa waziri wa hiyo wizara ni Harrison Mwakyembe.

Ni vizuri wanamichezo wote tukamuunga mkono Mwakyembe kwa kuwa kufanya hivyo tu ndiyo kunaweza kutusaidia kusonga mbele kwa michezo yetu.

Lazima tukubali kuwa Nape alifanya kazi nzuri na kila mmoja aliiona kazi yake, lakini kama ilivyokuwa kwa Nape naamini hata Mwakyembe anaweza kufanya mambo makubwa kama atapata ushirikiano kutoka kwetu kama ule tuliokuwa tukiimpa waziri aliyetangulia.

Nikiachana na haya ya Nape, leo nizungumzie mchezo wa Yanga dhidi ya MC Algier ya Algeria wa kutafuta nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Yanga hawana sababu yoyote ya kufanya vibaya kwenye mchezo huu, lakini kama ilivyo kawaida timu kutoka kwenye nchi za Kiarabu zimekuwa zikizisumbua sana timu za Tanzania.

Hii inamaanisha kuwa Yanga wanatakiwa kuwa makini kwa ajili ya maandalizi yao kutokana na fitina za timu za Kiarabu na wakati huohuo wajiandae wakiwa wanajua kuwa wanakwenda kupambana na timu bora kwenye bara hili la Afrika.

Timu hii ni kongwe kwani imeanzishwa mwaka 1922, hivyo ina ukongwe mkubwa kuliko hata Yanga ambayo imeanzishwa mwaka 1935, lakini ukubwa huu hauwezi kuisaidia timu hii kufanya vizuri uwanjani kama Yanga watajua kuwa wanakwenda kupambana na timu bora.

Yanga wanatakiwa kujua kuwa hapa wanapokwenda sasa walipita hapo msimu uliopita, hivyo wajue kuwa ili kufanya vizuri ni kuhakikisha kuwa wanakwenda kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri kuliko hatua ya makundi ambayo waliishia msimu uliopita.

Endapo Yanga watatolewa kwenye hatua ya nusu fainali kwa sasa hakuna ambaye atalalamika na kuwalaumu kwa kuwa wataona kuwa timu hiyo imefanya vizuri kuliko msimu uliopita.

Yanga wanatakiwa kujua kuwa kuonyesha wamekuwa ni kushinda mchezo huu na mingine inayofuata mbele.

Ukifuatilia rekodi ya timu hii inaonyesha kuwa ni timu bora sana ikiwa nyumbani kwao, hivyo kama Yanga ambao wanaanzia nyumbani wanataka kuhakikisha wanafuzu kwenye makundi basi watafute mabao mengi kwenye mchezo wa kwanza hapa nyumbani.

Inakumbwa kuwa kitendo cha sare ya bao 1-1 hapa nyumbani dhidi ya Zanaco ndiyo kimeiondoa timu hiyo ya Jangwani.

Kama Yanga wangetumia vizuri nafasi ambazo walizipata kwenye mchezo ule na kupata angalau mabao mawili leo tungekuwa tunazungumza mambo mengine kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Hivyo rai yangu ni kwa uongozi na benchi la ufundi la Yanga kuwajenga wachezaji wao kisaikolojia kuhakikisha kuwa wanafunga mabao mengi kwenye mchezo watakaocheza hapa nyumbani kwa kuwa ugenini kazi itakuwa ngumu.

Lakini ukiachana na hilo mashabiki wa Yanga wanatakiwa kujua kuwa wana sehemu kubwa sana ya ushindi wa timu yao.

Ni vyema wakawaunga mkono wachezaji wa timu hiyo wakati wakiwa uwanjani ili kuhakikisha kuwa timu hiyo inapata ushindi mnono hapa nyumbani.

Comments are closed.