The House of Favourite Newspapers

Yanga ya Kaze Kama Wafalme, Kukipiga na KMC Kirumba leo

0

MAPOKEZI waliyopewa Yanga ya Kocha Cedric Kaze walipotua jijini Mwanza hapo jana tayari kwa kuwavaa KMC leo Jumapili, ni kama wafalme fulani hivi.Yanga yenye pointi 16 kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, leo Jumapili itakuwa mgeni wa KMC katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

 

Baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege jijini Mwanza jana asubuhi, kikosi cha Yanga chenye wachezaji 26, kilipokewa na umati mkubwa wa mashabiki wa timu hiyo, kabla ya kuanza msafara wa kuelekea kwenye Hoteli ya Victoria Palace yenye hadhi ya nyota tatu iliyopo maeneo ya Capri Point kuweka mikakati ya ushindi.

Msafara huo wa mashabiki ulihusisha waendesha pikipiki maarufu bodaboda, magari binafsi pamoja na basi la timu hiyo ambalo lilibeba wachezaji na baadhi ya viongozi walioambatana na timu, huku mashabiki wengine wasiokuwa na usafiri wowote ambao walijazana kwa wingi barabarani wakiusindikiza msafara huo kwa macho.

Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh, ameliambia Spoti Xtra kuwa: “Kikosi chetu kimewasili salama jijini Mwanza na wachezaji wote wapo vizuri, wachezaji wana ari kubwa ya kupata ushindi dhidi ya KMC.

“Tumekuja kwa kazi moja tu ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zote zilizo mbele yetu kwa kukusanya pointi tisa hapa Kanda ya Ziwa kama kocha alivyoagiza.”

CARLINHOS AACHWA DAR

Katika msafara huo wa wachezaji 26, kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Carlos Carlinhos ameachwa jijini Dar sambamba na Balama Mapinduzi kutokana na wote kutokuwa fiti.

 

“Awali Carlinhos alikuwa anaendelea vyema na alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotakiwa kuja Mwanza, lakini amepewa mapumziko mengine baada ya kutokuwa vizuri kutokana na kuwa na maumivu ya kisigino na kupatwa homa, hivyo uongozi umeona ni vyema umpe mapumziko hadi atakapokaa vizuri huku akiendelea na matibabu,” alisema Hafidhi.

KAZE ABADILI MBINU

Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze raia wa Burundi, amesema wakiwa Kanda ya Ziwa ambapo watacheza mechi tatu, anataka kukusanya pointi zote tisa wakianza na tatu za leo dhidi ya KMC.

 

Lakini pia, kocha huyo anayesifika kwa kufundisha soka la kasi kwa kupiga pasi nyingi za chinichini, amesema wakiwa huko nje ya Dar kwenye viwanja ambavyo si rafiki sana, atabadilisha mbinu.“Kila mechi ina plani yake na mara nyingi zaidi inachangiwa na aina ya wachezaji ambao unao.

 

Lakini pia unaweza kubadili kutokana na viwanja.“Tukiwa viwanja vya mikoani ambavyo vingi si rafiki kucheza soka tunalotaka, tunapaswa kubadilisha mbinu za kiuchezaji, hivyo tutalazimika kucheza soka ambalo si la pasi zile za chini.

“Lakini pia, nafurahi kwa kufanikiwa kupata ushindi wangu wa kwanza nikiwa kama kocha mkuu wa kikosi cha Yanga, nakiri kuwa bado kikosi hakipo kwenye ubora ambao wote tunauhitaji, hivyo kama benchi la ufundi tuna kazi kubwa ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza.

 

“Tutaendelea kuweka msisitizo mkubwa kwenye programu zetu ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyonayo, naamini baada ya michezo mitano ijayo (sawa na dakika 450) tutakuwa na kikosi bora zaidi,” alisema Kaze.KMC

WANASEMAJE?

Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala, amesema: “Maandalizi ya kikosi chetu kuelekea mchezo dhidi ya Yanga yamekamilika kwa kiasi kikubwa, licha ya matokeo yasiyoridhisha kwenye michezo yetu minne iliyopita, lakini tuna uhakika asilimia 100 tutaondoka na pointi tatu.”

 

REKODI ZAORekodi zinaonesha kuwa, timu hizo zimekutana mara nne kwenye Ligi Kuu Bara ambapo Yanga imeshinda mechi mbili, KMC imeshinda moja na sare moja. Yanga imefunga mabao manne, KMC imefunga mabao matatu.

WAANDISHI: Khadija Mngwai, Joel Thomas na Said Ally

Leave A Reply