Yanga Yaanza Harakati Za Uwanja
KLABU ya Yanga imewaahidi mashabiki wake kuwa ipo kwenye mipango ya kuanza ujenzi wa uwanja wa mazoezi wa timu hiyo utakaofanyika Kigamboni pamoja na uzinduzi wa duka la vifaa vya mazoezi na jezi mpya zitakazozinduliwa hivi karibuni.
Jumapili Yanga ilifanikiwa kuhitimisha siku ya kilele cha wiki ya Mwananchi ambapo ilitambulisha wachezaji watakaotumika katika msimu wa mwaka 2020/21, katika siku hiyo Yanga ikifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir ya Burundi.
Akizungumza na Championi JumatanoOfisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz alisema kuwa viongozi wa timu hiyo wana madeni makubwa matatu ambayo ni ujenzi wa uwanja, uzinduzi wa duka pamoja na jezi mpya za timu hiyo.
“Tuna madeni matatu kwa Wanayanga ikiwemo jezi mpya, duka la vifaa, na ujenzi wa uwanja hivyo katika ujenzi wa uwanja tutakuwa na Kubwa Kuliko ambayo safari hii itakuwa kwa ajili ya mipango ya ujenzi wa uwanja huo ambayo utawezeshwa na Wanayanga wenyewe,” alisema Nugaz.
Kuhusu jezi alisema kuwa uzinduzi wa jezi utafanyika hivi karibuni na tutautangaza uzinduzi huo na Yanga itakuwa timu ya kwanza kuzindua duka la jezi kwenye makao makuu ya klabu.