The House of Favourite Newspapers

Yanga yabadili gia Zenji

0

YANGA (3)Wachezaji wa timu ya Yanga wakiendelea na mazoezi.

Suleiman Hassan, Pemba na Said Ally, Dar
MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga dhidi ya Azam FC, unaotarajiwa kupigwa kesho Jumamosi, unaonekana kuwa zaidi ya mchezo, kwani tayari presha imepanda kila upande lakini zaidi Yanga wameamua kwenda mbele zaidi kutokana na kubadili mbinu mbalimbali.

 
Ripoti kutoka kambi ya Yanga ambayo ipo Pemba, ilipoenda kabla ya kuichapa Simba mabao 2-0, zinaeleza kuwa licha ya Kocha Hans van Der Pluijm kuendelea na mazoezi kama kawaida, amekuwa makini na kujikuta akibadili programu ya mazoezi mara kadhaa huku ikielezwa kuwa yote hayo yanatokana na kukwepa mbinu za wapinzani wao.

SIMBA-YANGA-2.jpg
Tangu ifike Pemba, mwanzoni mwa wiki hii, Yanga ilikuwa ikiutumia Uwanja wa Gombani, kwa mazoezi ya asubuhi na jioni, juzi kulifanyika mabadiliko ambayo inaelezwa kuwa yalitokana na kuwavuruga mashushushu waliokuwa wakiwafuatilia.
Juzi Jumatano ilifanya mazoezi kuanzia saa 11:30 jioni wakati imekuwa na kawaida ya kufanya zaidi ya muda huo, katika mazoezi ya jana ilitegemewa kuwa mazoezi yangefanyika saa mbili asubuhi lakini badala yake yalifanyika saa nne asubuhi tofauti na kawaida yao.
“Kuna watu wanataka kuwafanyia ushushushu na mambo mengine ya kuwamaliza nje ya uwanja, ndiyo maana unaona kuna mabadiliko ya ratiba za mazoezi, wameshtukia mchezo mchafu.
“Hata leo (jana) kuna jamaa wanne walikuja Pemba moja kwa moja wakaja uwanjani, lakini walipoambiwa Yanga hawafanyi mazoezi jioni wakaondoka zao,” alisema mtu wa karibu wa timu hiyo ambaye yupo kambini Pemba.

YANGA (1)

Aidha, katika mazoezi hayo, Pluijm alionekana kuwa mkali na kutotaka utani, hali ambayo inaonyesha kuwa maandalizi ya mechi hiyo ni makali kama ambavyo imekuwa ikifanya pindi inapotarajiwa kukutana na Simba.
Hakukuwa na kiongozi wa Yanga aliyekuwa tayari kulizungumzia suala hilo.
Wakati huohuo, Kocha wa Azam, Stewart Hall, naye ameamua kufanya mabadiliko ya kimbinu na kimfumo kuelekea mchezo huo kwa kuwa timu yake imekuwa na matokeo ya kusuasua katika mechi za hivi karibuni.

 
Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd, ameliambia gazeti hili kuwa kocha wao ameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha timu inaibuka na ushindi.
“Kocha Hall anataka tuwafunge Yanga, hataki tena sare kama ilivyokuwa mechi ya kwanza, ndiyo maana ameamua kufanya mabadiliko hayo ambayo siwezi kuyazungumzia zaidi,” alisema Idd.
Yanga inaongoza ligi ikifuatiwa na Azam kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa lakini timu yoyote itakayopata ushindi itaongoza ligi kwa tofauti ya pointi na kujitengenezea mazingira ya kutwaa ubingwa.

Leave A Reply