The House of Favourite Newspapers

Yanga Yabanwa Mbavu na Kagera Sugar

0

LIGI kuu soka Tanzania bara iliendelea usiku wa leo 17 Februari 2021 kwa mchezo mmoja, vinara wa ligi hiyo, klabu ya Yanga ilicheza na wakata miwa kutoka mkoani Kagera, klabu ya Kagera Sugar na mchezo huo kumalizika kwa sare ya 3-3 kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kagera Sugar ndiyo ilikuwa ya kwanza kuziona nyavu dakika ya 11 kupitia kwa kiungo wake, Peter Mwaliyanzi kufuatia kujichanganya kwa Lamine Moro na Bakari Mwamnyeto wote kuwania mpira mmoja bila mahesabu mazuri ya kujipanga na kumnufaisha Mwaliyanzi.

Yanga ambayo ilikuwa inasheherekea miaka 86 ya kuanzishwa kwake, walirudi mchezoni baada ya kusawazisha dakika ya 14 kwa mkwaju wa penalti kupitia winga wake Tuisila Kisinda na ndipo Kagera wakajibu mapigo na kupata bao la kuongoza kupitia mshambuliaji wake Hassan Mwaterema dakika 24.

Mchezo ukawa wa mashambulizi ya wazi ya piga nikupige kwani Yanga walisawazisha tena kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji, Deus Kaseke dakika ya 30 na kuwashtua Kagera Sukari. Kabla ya mapumziko, aliyekuwa mchezaji wa Yanga, Yusuf Mhilu alifunga bao la tatu kwa Kagera Sugar.

 

Dakika ya 60, Mukoko aliisawazishia Yanga kwa shuti la umbali mrefu baaada ya kugongeana pasi na Ditram Nchimbi na kufanya matokeo kuwa 3-3.

Yanga baada ya sare hiyo bado inaendelea kuogoza ligi kwa kufikisha alama 46, na kujiweka kwenye mazingira magumu kwani endapo Simba ikishinda mechi zake tatu itakwea kileleni kwa tofauti ya alama 2.

Leave A Reply