The House of Favourite Newspapers

Yanga Yafikishwa Kamati ya Sheria TFF

 

KUFUATIA madai ya waliokuwa wachezaji watatu wa Klabu ya Yanga kufikisha malalamiko yao katika Chama cha Haki za Wachezaji Tanzania (Sputanza), klabu hiyo imejikuta ikifikishwa katika Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji (TFF) kujibu mashitaka.

 

Wachezaji ambao walifikisha malalamiko yao Sputanza ni pamoja na Pato Ngonyani, Mwinyi Haji na Antony Matheo ambao wanadai fedha zao za mishahara na usajili.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mwenyekiti wa Sputanza, Mussa Kisoki amesema wamepokea malalamiko kutoka kwa wachezaji hao ambapo tayari wameshayawasilisha kwa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao kwa ajili ya kufanyia kazi.

 

“Pato, Mwinyi Haji na Matheo walifika hapa hivi karibuni kuleta barua yao kudai fedha zao za mishahara ya miezi miwili pamoja na fedha za usajili na tayari tumeshalifikisha suala hilo kwa katibu mkuu TFF, hadi ninapozungumza hapa tayari uongozi wa Yanga umeshafikishiwa barua.

 

“Pia suala hili litafikishwa katika Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za wachezaji ili kuwaita wahusika ambao ni Yanga waweze kufikia muafaka wa kuwalipa wachezaji hao.

 

“Lengo letu ni kuona wachezaji wote wanapatiwa haki zao za msingi pia wachezaji wanatakiwa kulipwa fedha zao za usajili pindi wanaposajiliwa tu na si vinginevyo, hivyo mchezaji yeyote yule mwenye matatizo wanakaribishwa ili yafanyiwe kazi,” alisema Kisoki.

 

Aidha, Championi Ijumaa lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela ambaye alisema: “Suala hilo limetufikia, tunajua wachezaji hao wanatudai haki zao, tupo katika mchakato wa kuwalipa, deni lao ni miongoni mwa madeni tuliyorithi.”

Comments are closed.