The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaifukuzia Rekodi Simba

0

BAADA ya ushindi wa mabao 3-1 walioupata Yanga katika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji, unaambiwa timu hiyo imebakisha michezo 5 tu ili kuifikia rekodi inayoshikiliwa na Simba kwa sasa ya kucheza michezo mingi ya ligi kuu bila kupoteza.

 

Yanga baada ya ushindi huo, sasa wamefikisha idadi ya michezo 28 ambayo wamecheza bila kupotea hata mchezo mmoja, jambo ambalo linawafanya kusaliwa na michezo mitano tu ili waweze kuifikia rekodi hiyo ya Simba.

 

Simba wanashikilia rekodi ya kucheza michezo 33 bila kufungwa ambayo waliiweka kuanzia Aprili 10, 2017 hadi Mei 12, 2018, rekodi ambayo haijafikiwa na timu yoyote ya ligi kuu tangu waiweke wao.

 

Kwa upande wa Yanga ambao wameweka rekodi ya kutopoteza mchezo wowote katika michezo 28, rekodi hiyo waliiweka kuanzia Machi 15, 2020 yaani mwisho wa msimu uliopita mpaka Jumamosi Desemba 19,2020 walipoifunga Dodoma Jiji kwa mabao 3-1.

 

Yanga mara ya mwisho kupoteza mchezo wa ligi kuu ilikuwa katika msimu uliopita, Machi 12, 2020 walipofungwa na KMC kwa bao 1-0, lililofungwa na Salim Aiyee kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar, tangu hapo hawajapoteza tena mchezo wowote wa ligi hiyo.

 

Yanga kwa sasa ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa wanaongoza ligi hiyo mara baada ya kufanikiwa kukusanya pointi 40 katika michezo 16 waliyocheza wakiwa wameshinda michezo 12 na kutoa sare nne.

 

Hata hivyo, Yanga wanaitafuta rekodi nyingine ya Simba ya msimu wa 2009/10 ambapo walicheza msimu mzima bila kupoteza mchezo wowote ambapo walicheza michezo 22 bila kufungwa.

MARCO MZUMBE, Dar es Salaam

Leave A Reply