Yanga Yaifungia Namungo Full Mziki Kesho Kwenye Uwanja wa Ruangwa Lindi
MSAFARA wa wachezaji 21 wa Yanga umesafiri kuelekea mkoani Lindi, kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC utakaochezwa kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Ruangwa.
Katika msafara huo, wamejumuishwa Fiston Mayele, Dickson Job na Jesus Moloko ambao juzi walikosekana wakati Yanga ikiifunga Prisons bao 1-0.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, alisema anafurahi kuona Job, Moloko na Mayele kurejea kikosini.
Nabi alisema kurejea kwa nyota hao kutaimarisha safu ya ulinzi na ushambuliaji.
Aliwataja wachezaji watakaosekana katika mchezo huo ni Salum Aboubakari ‘Sure Boy’ na Farid Mussa.
“Hatutafanya mzaha katika kila mchezo ulipo mbele yetu, tukianzia mchezo ujao tutakaocheza dhidi ya Namungo ambao ni lazima tupate ushindi ili tuendelee kukaa kileleni.
“Nimewaona na kuwafuatilia kwa karibu Namungo katika michezo iliyopita nikiwa pamoja na msaidizi wangu Kaze (Cedric) ambaye yeye ndiye atakaa katika benchi kuiongoza timu.
“Kuelekea mchezo huo nina furaha kuwaona wachezaji wangu watatu muhimu ambao walikosekana katika mchezo huu ambao ni Mayele, Moloko na Job, ninaamini uwepo wao utaongeza ubora wa kikosi changu,” alisema Nabi.