Yanga Yaisogeza Mbele Siku ya Mwananchi

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umeisogeza mbele Siku ya Mwananchi ambayo hapo awali ilipangwa kilele chake kufanyika Julai 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku pia ukiweka wazi kuwa kikosi chao kitacheza mechi tano za kirafiki kabla ya kuanza msimu mpya.

 

Katika siku hiyo, uongozi wa Yanga umepanga kuwatambulisha wachezaji wao wapya na kucheza mchezo wa kirafiki. Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten, amesema sherehe hizo zimesogezwa mbele kupisha mchezo wa kimataifa wa Taifa Stars dhidi ya Kenya utakaopigwa Julai 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa ukiwa ni wa kuwania nafasi ya kushiriki mashindano ya Chan.

 

“Wanayanga watambue kuwa Siku ya Mwananchi haijafutwa ila imesogezwa mbele na tutatangaza tarehe nyingine ndani ya wiki hii,” alisema Ten na kuongeza: “Kambi yetu iliyopo Morogoro inaendelea vizuri na wachezaji karibia wote wanaendelea na mazoezi, wale ambao walikuwa na timu ya taifa wataingia kambini Julai 14.

 

Benchi la ufundi limepanga kucheza michezo mitano ya kirafiki kwa lengo la kukipima kikosi chetu kipya. Julai 15 na 19 tutacheza pale Morogoro na timu ambazo tutazitangaza hivi karibuni, lakini Julai 23 tutakwenda Dodoma kucheza na Dodoma FC, kisha Julai 30 tutakwenda Ifakara kuvaana na Ifakara FC. “Baada ya hapo, timu itakuwa inajiandaa kurejea Dar es salaam kujiandaa na msimu mpya.” Aidha Ten alisema, tayari majina ya wachezaji wao 23 wameyatuma Caf kwa ajili ya michuano ya kimataifa.

Loading...

Toa comment