The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaitikisa Al Merrikh, Injinia Hersi Afunguka Mipango Ya Kuimaliza – Video

0

JIONI ya Septemba 14, 2023 Alhamisi, kikosi cha Yanga kitasafiri kwa ndege kuelekea Kigali, Rwanda, tayari kwa mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza dhidi ya Al Merrikh.

Wakati kikosi cha Yanga kikitarajiwa kutua Rwanda usiku wa leo, tayari wenyeji wao, Al Merrikh wametikisika baada ya kuona hamasa kubwa iliyopo kwa mashabiki wa Yanga waliopanga kuipa sapoti timu yao siku ya mchezo utakaopigwa Septemba 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kigali Pelé uliopo Rwanda.

Zaidi ya mabasi 28 yanatarajiwa kutoka Tanzania kwenda Rwanda yakiwa na mashabiki wa Yanga, ambao wanakwenda kuisapoti timu yao irudi na ushindi kwa lengo la kupata nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kuikosa nafasi hiyo kwa takribani miaka 25 kwani mara ya mwisho kucheza hatua hiyo ni mwaka 1998.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Rwanda, Al Merrikh ni kama wana hofu kubwa ya kupambana na Yanga baada ya kuona wapinzani wao wanakuja na mashabiki lukuki.

“Hapa Rwanda gumzo kubwa ni namna Yanga wanavyokuja na mashabiki wao, hamasa inaonekana kuwa kubwa kwa Yanga kuliko hata Al Merrikh ambayo imeamua kutumia uwanja wa hapa kwa mechi zao za nyumbani baada ya kwao Sudan hali kutokuwa nzuri.

“Al Merrikh wanajiona kama wapo ugenini wakati Yanga wakionekana wanakuja kucheza nyumbani kutokana na hamasa ya mashabiki wao ilivyo,” alisema mtoa taarifa wetu.

MASTAA YANGA WALA KIAPO
Kuelekea mchezo huo, Maxi Nzegeli ambaye ni nyota wa Yanga, amesema malengo yao kama timu ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri wakiwa ugenini ili mchezo waumalizie hukohuko kabla ya kurudiana Dar.

“Tunahitaji kupata matokeo mazuri tukiwa ugenini ili safari yetu ya kwenda hatua ya makundi iwe rahisi kwa kuwa kama tutashinda ugenini basi hatutakuwa na ugumu sana tukiwa nyumbani.

“Tunafahamu ugumu wa mchezo huu, lakini siku zote Ligi ya Mabingwa Afrika haijawahi kuwa na mechi nyepesi kwa kuwa ni mabingwa ambao hukutana,” alisema nyota huyo.

Kwa upande wa Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, amesema: “Tupo tayari kwa ajili ya mchezo wetu ambao utachezwa Rwanda, tunaitaka hatua ya makundi, hivyo mashabiki na Watanzania kwa jumla wazidi kuwa pamoja nasi.”

Naye kipa wa Yanga, Metacha Mnata, alisema maandalizi ambayo wameyafanya ni kwa ajili ya kupata matokeo mazuri popote pale iwe ugenini au nyumbani.

Leave A Reply