BAADA ya Yanga kuanza vibaya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi na kuburuza mkia wa Kundi D, kaimu kocha mkuu wa kikosi hicho, Noel Mwandila raia wa Zambia, ameibuka na kusema wanahitaji pointi 10 ili waingie robo fainali.
Yanga ambayo imepangwa Kundi D na timu za USM Alger ya Algeria, Gor Mahia (Kenya) na Rayon Sports kutoka Rwanda, inaburuza mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi mbili, imepoteza moja na kutoka sare moja.
Katika kundi hilo, USM Alger inaongoza ikiwa na pointi nne, huku Gor Mahia na Rayon zikiwa na pointi mbili. Timu hizo zote zimecheza mechi mbili mpaka sasa, huku zote zikibakiwa na mechi nne za hatua ya makundi.
Juzi Jumatano, Yanga ililazimishwa suluhu na Rayon Sports katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, ambapo Mwandila amesema ni lazima wakusanye pointi 10 au zaidi kwa lengo la kusonga hatua inayofuata.
“Sijafurahishwa na matokeo haya kwani matarajio yetu yalikuwa ni kuona tunashinda mchezo huu kutokana na kucheza nyumbani, kwa bahati mbaya hatukuweza kupata ushindi.
“Kilichobaki sasa ni kushinda mchezo ujao wa ugenini na mingine ya nyumbani iliyobaki, tunataka kufikisha pointi kumi au zaidi ili tuvuke hatua hii, tunaamini bado tuna nafasi ya kufuzu,” alisema Mwandila.
Stori: Omary Mdosen a Said Ally
Comments are closed.