The House of Favourite Newspapers

Yanga Yakumbana na Aibu ya Mwaka CAF

KWA mujibu wa rekodi za ndani za CAF, Yanga inachodai sasa ni Sh.Milioni 311 tu baada ya awali kupewa advansi ya Sh.312Milioni ili iweze kushiriki vizuri michuano hiyo. Lakini matarajio yakaenda kinyume wakajikuta wakikumbana na aibu ya aina yake kwenye hatua ya makundi ya Kombe hilo la Shirikisho ambalo klabu nyingi zimekuwa zikitamani kucheza.

 

Hatua hiyo ya makundi ilivyopangwa mashabiki wa Yanga walishangilia na kudai kwamba msimu huu wangecheza hata nusu fainali, lakini kibao kimegeuka uwanjani na timu yao kujikuta iking’ang’ania mkiani mwa Kundi D. Haitaki kung’atuka kwenye nafasi hiyo tangu makundi yameanza. Yanga ndiyo timu pekee kwenye hatua hiyo ambayo mpaka sasa ina pointi moja tu katika mechi nne ilizocheza.

 

Mshindi wa tatu na wa mwisho kila kundi hupewa Sh.Milioni 623 ambapo kwa hali ilivyo mpaka sasa hata ikishinda mechi zilizobaki haiwezi kusogea zaidi ya nafasi ya tatu. Mbali na pointi yake moja, Yanga ambayo imepangwa na timu mbili za ukanda wa Cecafa ambazo ni Gor Mahia ya Kenya na Rayon ya Rwanda, ndiyo timu pekee iliyoruhusu mabao 11 katika mechi nne ambayo ndiyo mengi zaidi kwenye makundi yote.

 

Siyo hilo tu, rekodi ambayo Yanga mbovu nyingine ambayo inaweza kujitetea nayo ni ile ya kutokushinda mechi hata moja mpaka sasa kama ilivyo pia Rayon walioko naye kwenye kundi moja.

 

Rayon na mwenyewe aliingia kwenye mashindano hayo kwa mbwembwe nyingi za mdomoni kama Yanga lakini vitendo vya uwanjani vikagoma. Timu nyingine ambazo hazijashinda mechi yoyote kwenye hatua hiyo ya makundi mpaka sasa ni UD Songo ya Msumbiji na Al Hilal ya Sudan zilizoko kundi B ambayo straika Mtanzania,Thomas Ulimwengu amejiunga nayo hivi karibuni baada ya kukosa timu kwa kipindi kirefu.

 

Klabu maarufu ya Asec Memosas ya Ivory Coast iliyoko Kundi A imepoteza mechi tatu kama Yanga lakini ina pointi tatu iking’ang’ania kwenye nafasi ya mwisho katika kundi lake.

 

Yanga imepachika mabao mawili tu tangu michuano hiyo ianze kama ilivyo kwa Asec. Mashabiki wengi wa Yanga walitarajia kwamba ingeweza kufuzu kirahisi hatua ya robo fainali kutokana na uwepo
wa Rayon na Gor M ahia kwenye kundi lake.

 

Kwa pointi moja iliyoambulia Yanga ni ndoto kufuzu hatua hiyo kutokana na mechi mbili walizosaliwa nazo dhidi ya USM Algiers na Rayon ambazo hata wakishinda watakomea pointi saba ambazo Gor Mahia ameshazivuka. Rayon yenye pointi tatu ina uwezo wa kuvuka kama itashinda mechi zake mbili zilizobaki.

 

Yanga kama ingetwaa ubingwa huo msimu huu ingejihakikishia kushiriki michuano ya kimataifa Novemba kwa kuchukua nafasi ya Mtibwa, lakini kwa kilichotokea watalazimika kwenda Taifa kuishangilia Simba wakisubiri bahati yao msimu wa 2019/20. Kwa taratibu za CAF zilivyo bingwa mtetezi akitokea kwenye nchi yenye mwakilishi mmoja, basi mwakilishi husika atapaswa kukaa pembeni kumpisha bingwa atetee kombe lake.

Comments are closed.