The House of Favourite Newspapers

Yanga Yakwama Kwa Ndemla

0
Kiungo wa Simba, Said Ndemla.

KIUNGO wa Simba, Said Ndemla amekwenda kwenye majaribio nchini Sweden kwa siku 14, lakini Yanga imekwama kumsajili kutokana na mambo kwenda tofauti na ilivyotarajia. Juzi Ndemla alisafiri kwenda Sweden kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya AFC Eskelistuna inayomuhitaji.

 

Wakati Ndemla akiwa katika harakati za kwenda Sweden, habari zinasema Yanga ilitaka kutumia kipindi hicho kumsajili ikiamini amebakisha siku 14 tu katika mkataba wake. Licha ya kuwa katika uwezo wa kuzungumza na klabu yoyote kwa kujiunga nayo, Simba inaonekana wazi haipo tayari kuvunja mkataba wa Ndemla ili ajiunge na Yanga.

Kikosi cha Yanga.

Hilo lingewezekana endapo kweli ingekuwa Ndemla amebakiza siku 14 za mkataba wake na Simba kwani angesajiliwa kama mchezaji huru. Yanga ilitaka kufanya kama lile tukio la beki wake Ramadhan Wasso aliyetimkia Simba kwa kisingizio cha kwenda nje ya nchi kwa majaribio.

 

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Yanga iliamini mkataba wa Ndemla unamalizika ndani ya siku 14 ambazo amepewa kwa ajili ya kufanya majaribio Sweden.

 

Klabu hiyo inaelezwa kuwa, baada ya siku 14 hizo kumalizika akiwa Sweden, basi mabosi wa Yanga walipanga kumpa mkataba wa miaka miwili kiungo huyo. Lakini ukweli ni kwamba Ndemla ana mkataba wa miezi minne na Simba na japokuwa anaruhusiwa kuzungumza na timu nyingine ila ni ngumu kwake kutosa dili hilo la Sweden. Usajili wa dirisha dogo utafunguliwa Novemba 15 na utafungwa Desemba 15, mwaka huu ambapo timu za Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza zitahusika.

 

Mmoja wa mabosi wa Simba, aliliambia Championi Jumamosi kuwa; “Ndemla ana mkataba wa miezi minne Simba, yaani amebakisha miezi minne katika mkataba wake, sasa Yanga wanadhani kabakisha siku 14, wanajidanganya kwani hawataweza kumpata.

 

“Tuna uhakika atafanya vizuri katika majaribio na tutamuuza hivyo ndoto za Yanga kumsajili ni kujidanganya tu, tupo makini katika usajili sasa kuliko siku za nyuma.” Mmoja wa watu wa karibu wa Ndemla amesema, licha ya timu anayoenda kufanya majaribio kiungo huyo kushuka daraja kutoka Ligi Kuu ya Sweden, sasa inasukwa upya ili iweze kufanya vizuri katika Daraja la Kwanza na kurejea ligi kuu.

 

“Wale jamaa wanataka kiungo na tuna uhakika Ndemla atafanya vizuri na kusajiliwa kwa hali yoyote ile, sasa hapo Yanga haitaweza kumpata kwani haitaweza kuwa na fedha za kuipiku timu ya Ulaya,” alisema rafiki wa Ndemla.

 

Championi Jumamosi lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika kuzungumzia hilo, lakini simu yake iliita bila ya kupokelewa lakini Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa yeye alisema: “Siwezi kuzungumzia hilo kwa sasa kwani usajili bado haujafunguliwa.”

 

Kwa upande wa Simba, viongozi wengi hawakuwa tayari kupokea simu zao na kutoa ushirikiano lakini mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally alisema: “Hizo habari za Yanga sizijuhi na sisi tunatambua Ndemla ni mchezaji wetu japokuwa mkataba wake unaelekea ukingoni.” Katika siku za nyuma, mmoja wa viongozi wa zamani wa Simba aliwahi kusema kuwa Ndemla yupo njiani kuelekea Yanga pindi atakapomaliza mkataba.

Stori: Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge

Leave A Reply