The House of Favourite Newspapers

Yanga Yamsindikiza Wambura kuanza kazi TFF

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Michael Wambura.

BAADA ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kumrejesha rasmi aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Michael Wambura kiongozi huyo ataripoti rasmi ofisini keshokutwa Jumanne, kuanza kazi. Rais wa TFF, Walace Karia alisema jana mjini Tanga kwamba hawawezi kuzungumzia lolote kuhusu Wambura mpaka wakutane. Lakini habari zilizokuwa zinazungumzwa jana Jumamosi na wanachama wa Yanga klabuni ni kwamba watamuunga mkono jumanne siku ambayo anarejea kwenye ofisi za TFF.

 

Ingawa haikufafanuliwa zaidi lakini Spoti Xtralimegundua kwamba wanamuunga mkono Wambura kutokana na kumtuhumu mmoja wa vigogo wa TFF kwamba anakoleza moto kwenye uchaguzi wao na kutaka nafasi ya Yusuf Manji ijazwe.

 

Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimrejesha Wambura katika vyeo vyake baada ya kupitia malalamiko yake mbele ya Jaji Benhaji Masoud ni baada ya kuomba kupitiwa maamuzi ambayo yalitolewa na kamati ya maadili ya TFF.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Wakili wa Wambura, Emmanuel Muga alisema; “Wambura kwa sasa yuko huru kabisa na tunatarajia kuwa mambo yakienda sawa siku ya Jumanne ataripoti kazini kwake pale TFF mara moja na kuanza kazi.” “Pale ataanza kazi yake na kwa sababu yeye ni bosi hahitaji kuripoti kwa mtu yoyote pale zaidi wafanyakazi wenzake wanatakiwa tu kumkaribisha tu sababu hawakuwa naye kwa muda mrefu,”alisema Muga.

 

Machi mwaka huu Kamati ya Maadili ya TFF chini ya mwenyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni ilimfungia maisha Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa kumtuhumu kwa makosa matatu. Katika taarifa yake, TFF ilisema kwamba ilichukuwa hatua hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013.

 

Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye Kamati hiyo kwa tuhuma za makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi barua na kushusha hadhi ya TFF.

Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF iliyodai baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura ilionekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.

STORI NA MARTHA MBOMA | SPOT XTRA

Simba waondoka kibabe usiku mnene kuifata mbabane swallows

Comments are closed.