The House of Favourite Newspapers

Yanga yamuombea ulinzi Ngoma

0

Donald-Ngoma-1

Straika wa Yanga, Donald Ngoma.

Khadija Mngwai,Dar es Salaam
UONGOZI wa Yanga umelijia juu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kutompa ulinzi wa kutosha straika wake, Donald Ngoma, kufuatia kuchezewa rafu mbaya mara kwa mara kwenye mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu.

Ngoma ambaye amejiunga na Yanga msimu huu akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, amekuwa kwenye wakati mgumu katika msimu wake wa kwanza akiwa Ligi Kuu Bara, kutokana na mabeki wa timu pinzani kumkamia kila wanapocheza dhidi yake.

Akizungumza na Championi Jumatano, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, amefunguka kuwa, kwa sasa wachezaji wa Yanga, hasa Ngoma, ndiyo wanaongoza kwa kuchezewa rafu nyingi zaidi tena za makusudi huku pia wakiongoza kwa kupewa kadi nyingi na adhabu za kulipishwa fedha, tofauti na wapinzani ambao ndiyo huwa na makosa.

Alisema itafika wakati wataomba wahusika wanaosimamia vitu hivyo kujiuzulu kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo masuala ya wachezaji kwani wamechoshwa na hali hiyo.

“Kwa sasa hatuhitaji kusema kitu chochote kuhusiana na jambo hilo kwani tukisema tutaonekana tunachagua waamuzi wa kuchezesha mechi zetu ambao wakati mwingine hawatendi haki.

“Vijana wetu wanajikuta wanapewa kadi nyingi za njano katika mechi tunazocheza tofauti na timu pinzani ambapo hata wachezaji wetu wakichezewa rafu, refa amekuwa akiacha tu tofauti na ilivyo kwa wengine, upande wetu hata kosa likiwa dogo wanapewa, sijajua kama ni mipango ama la.

“Itafika wakati tutaomba wahusika wa vitu hivyo wajiuzulu kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo masuala ya wachezaji kwani tumechoshwa na hali hii, wachezaji wetu wamekuwa hawana amani.

“TFF ndiyo inayotakiwa kulinda wachezaji wasichezewe rafu, lakini wamekaa kimya ipo siku tutazungumza kuhusiana na hili, kwa sasa tunasubiri hatutaki kuzungumza,” alisema Tiboroha.

Aidha alimalizia kwa kusema kuwa, wataanza maandalizi dhidi ya Azam baada ya mechi ya timu ya taifa na Malawi kuhakikisha wanawafunga wapinzani wao hao.
Ngoma na Amissi Tambwe ndiyo vinara kwa mabao kwenye kikosi cha Yanga huku kila mmoja akiwa ameshapachika mabao manne kwenye ligi hiyo ambayo imeanza hivi karibuni.

Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye mchezo kati ya Simba na Yanga, Ngoma alichezewa rafu nane na mbili kati ya hizo zilizaa kadi za njano.

Leave A Reply