The House of Favourite Newspapers

Yanga Yapata Vikosi Viwili Kamili

0

KOCHA Mkuu wa Yanga Mserbia, Zlatko Krmpotic, tayari ametengeneza vikosi viwili vya timu hiyo katika kupata kimoja ambavyo juzi alivitumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mlandege ya Zanzibar.

 

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, Mbagala nje kidogo ya jiji la Dar ulimalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Waziri Junior, Mukoko Tonombe.

 

Katika mchezo huo, kocha huyo alitumia vikosi viwili alivyovigawa ambavyo vilicheza kipindi kimoja sawa na dakika 45, kila timu ikifanikiwa kupata bao pekee.

Kikosi cha kwanza kilichoanza, kilifunga bao kwa njia ya penalti kupitia kwa mshambuliaji Wazir Junior. Penalti hiyo ilipatikana baada ya nahodha na kiungo mchezeshaji Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, kupiga krosi ambayo iliishia mkononi mwa beki wa Mlandege na mwamuzi wa kati kupiga kipyenga cha penalti.

 

Kikosi hicho kilichoanza kilikuwa hivi; kipa Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Adeyuma Saleh, Said Makapu, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Abdulaziz Makame, Niyonzima, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Ditram Nchimbi, Junior na Farid Mussa.

 

Wakati kikosi cha kilichoingia kipindi cha pili kiliundwa na Ramadhani Kabwili, Deus Kaseke, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya, Carlos Fernandes ‘Carlihnos’, Mukoko Tonombe, Michael Sarpong, Yacouba Songne na Tuisila Kisinda.

 

Kikosi hicho kilichoingia kipindi cha pili, bao lao lilifungwa na Tonombe ambaye alipokea pasi ya Yacouba kabla ya Tonombe kupiga shuti kali nje kidogo ya 18 na kutinga wavuni.

 

Katika mchezo huo, kikosi hicho cha pili kilionekana kucheza vizuri kutokana na kupiga pasi nyingi na kuutawala mchezo huo katika safu ya kiungo iliyokuwa inachezwa na Mauya na Tonombe waliokuwa wakitawanya mipira kwa washambuliaji.

 

Yanga iliutumia mchezo huo wa kirafiki katika kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar watakaocheza kesho kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera wenye nyasi bandia kama ulivyokuwa wa Azam Compelex.Hii inaonekana kuwa sasa kocha wa Yanga anachaguo la kupata kikosi kitachocheza kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply