Yanga yapeleka nguvu zake za usajili Ethiopia
Hans Mloli,
Dar es SalaamK
LABU ya Yanga awali ilitangaza haina mpango wa kusajili katika kipindi hiki cha dirisha dogo lakini ukweli ni kwamba imeweka mitego yake kuangalia ‘majembe’ ya uhakika kwenye michuano ya Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Michuano hiyo inatarajia kuanza Novemba 21 na kumalizika Desemba 6, mwaka huu nchini Ethiopia.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, amezungumza na Championi Jumatano na kufunguka kuwa, benchi la ufundi la timu hiyo, limeamua kutokurupuka na usajili wa wachezaji wa timu za Ligi Kuu Bara kwa tathmini ya kukosa viwango vya ushindani dhidi ya wachezaji waliopo Jangwani kwa sasa, hivyo wameamua kusubiri kuangalia kama wanaweza wakanasa saini ya ‘fundi’ yeyote kwenye michuano hiyo.
Aidha, alitiririka kuwa katika hilo wanamsikiliza kocha wao Mholanzi, Hans van Der Pluijm, kama ataridhika na mchezaji yeyote wao watakuwa hawana njia zaidi ya kukamilisha usajili na kuendelea kutengeneza kikosi chao.
“Ni kweli kocha Pluijm hakuna zoezi lolote la usajili aliloliwasilisha mezani mpaka sasa na zaidi tunatarajia kuangalia kama kutakuwa na lolote jipya katika Chalenji, maana kule kunakuwa na wachezaji kutoka sehemu tofautitofauti.
“Sisi tutamsikiliza yeye (Pluijm), kama atakuwa na mapendekezo yoyote aliyoyaona Chalenji basi tutakamilisha mara moja hayo masuala, maana dirisha ndiyo kwanza limefunguliwa juzi kwa hiyo tuna kipindi kirefu bado,” alisema kiongozi huyo.
Dirisha la usajili lilifunguliwa Novemba 15 na linatarajiwa kufungwa Desemba 15, mwaka huu na tayari timu mbalimbali zimeshaanza harakati za kuboresha vikosi vyao.