The House of Favourite Newspapers

Yanga yasajili kiboko ya Niyonzima

0

issoufou-boubacar2Mshambuliaji, Issofou Boubacar.

Wilbert Molandi,
Dar es Salaam
KATIKA usajili wa dirisha dogo uliofikia tamati Desemba 15, mwaka huu, Yanga imesajili wachezaji wawili tu, straika Paul Nonga na kiungo mshambuliaji, Issofou Boubacar ili kujiimarisha.

NIYONZIMANEW4Haruna Niyonzima.

Lakini jana Ijumaa asubuhi katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Boko Veterani, Yanga ilianza kumfanyia majaribio kiungo Sina Jerome aliyetokea Rayon Sports ya Rwanda.
Yanga inafanya hivyo ili kujiridhisha kuhusu uwezo wa Jerome mwenye umri wa miaka 26 halafu imsajili ili imtumie katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika kwani haitaweza kupeleka jina lake Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili imtumie katika Ligi Kuu Bara kwa kuwa muda umepita tangu Desemba 15, mwaka huu.
Pia Yanga inaelezwa inamsajili kiungo huyo ili kuziba nafasi ya Haruna Niyonzima ambaye imemsimamisha kwa muda usiyojulikana kwa madai ya utovu wa nidhamu wa kuchelewa kurejea nchini kutoka kwao Rwanda.
Hata hivyo, habari kutoka Rwanda zinadai Jerome pia ana tatizo la kinidhamu, hivyo Yanga inatakiwa kuwa makini naye kwani utoro kama wa Niyonzima unaweza ukawa tatizo kwao.
Katika mazoezi ya jana, Jerome aliyezaliwa Februari 18, 1989 alifanya vizuri kiasi cha kuwavutia mashabiki na benchi la ufundi ambapo wengi wao walionekana kusikitikia ujio wa kiungo huyo kwani kama angewahi angeongezwa kwenye kikosi cha ligi kuu.
Akiwa katika mazoezi hayo, mchezaji huyo anayemudu kucheza kiungo cha kukaba na kushambulia inapobidi, alionyesha uwezo mkubwa wa kufunga kwani alifunga mabao manne na kutengeneza mawili.
Kiungo huyo raia wa Rwanda, alionyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga mashuti makali kutoka nje ya eneo la hatari la adui huku akitumia miguu yote kufanya hivyo.
Chanzo kutoka Kamati ya Utendaji ya Yanga, kimesema kiungo huyo ameletwa na mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbagu ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo.
“Kiungo huyu ameletwa ili akifaa acheze mechi za Caf (Shirikisho la Soka Afrika), maana wao wana usajili tofauti na huu wa ligi kuu kwani bado haujafungwa,” kilisema chanzo hicho. Usajili wa Caf bado unaendelea hadi Desemba 31, mwaka huu.
Akimzungumzia kiungo huyo, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, alisema: “Kiungo huyu amekuja kwa majaribio na akifuzu tunamsajili, ila kwa leo tu nimemuangalia kwa muda mfupi na nimefurahishwa na uwezo wake.
“Ni kiungo mzuri anayeweza kumiliki mpira, kupiga pasi na hata kufunga.”

Leave A Reply