The House of Favourite Newspapers

Yanga Yateketeza Bilioni 1.1 Kwa Nyota Saba

0

KATIKA kuhakikisha wanakisuka kikosi chao, Yanga itatumia kitita cha Sh bilioni 1.1 kufanikisha usajili wa wachezaji saba tishio katika msimu ujao.Yanga imepanga kufanya kufuru ya usajili katika msimu ujao.

 

Timu hiyo hivi sasa inaendelea na usajili wa kimyakimya kwa hofu ya kuzidiwa ujanja na watani wao Simba kama ilivyotokea kwa Luis Miquissone raia wa Msumbiji na Mzambia Larry Bwalya.

 

Mchezaji aliyetangazwa kusajiliwa na Yanga hadi hivi sasa ni beki wa kulia wa AS Vita Mkongomani, Shaban Djuma ambaye usajili wake ulifanikishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, Injinia Hersi Said.

 

Usajili wa Djuma ni Sh milioni 500 ambaye atajiunga na Yanga katika msimu huu kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na AS Vita kumalizika.Yanga itaingia gharama nyingine kubwa ya Sh milioni 231 kumsajili kiungo mshambuliaji wa Union Maniema ya DR Congo, Mercey Vumbi Ngimbi ambaye yeye anataka kujiunga na timu hiyo baada ya kushawishiwa na Wakongomani Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe.

 

Ngimbi hivi karibuni aliingia kwenye vita kubwa ya kuwaniwa na Yanga na TP Mazembe ambayo ilitupa ndoano kuwania saini ya kiungo huyo mwenye kasi.

 

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga anayekipiga Horoya AC ya nchini Guinea naye anatarajiwa kukomba kitita cha Sh milioni 200 ili asitishe mkataba wake wa mwaka mmoja alioubakisha katika timu hiyo.

 

Makambo ameonyesha nia kubwa ya kujiunga na Yanga ambaye hivi sasa anawasubiria mabosi wa timu hiyo kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya mwisho kabla ya kuandika barua ya kusitisha mkataba.

 

Dickson Ambundo ambaye ni kiungo mshambuliaji wa Polisi Tanzania naye amemalizana kwa asilimia kubwa na mabosi wa timu hiyo na atajiunga kwa mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh 50Mil.

 

Mshambuliaji wa Mbeya City, Denis Kibu inasemekana amesaini mkataba wa awali wa kuichezea Yanga kwa dau la Sh 80Mil baada ya kufikia muafaka mzuri na mabosi wa Yanga kwa mkataba wa miaka miwili.

 

Beki wa kushoto wa KMC FC, David Bryson naye anatajwa kufikia muafaka mzuri na Yanga ambaye amepewa mkataba wa awali wa miaka miwili kwa dau la Sh 50Mil.

 

Beki huyo atajiunga na timu hiyo kwa ajili ya kuiboresha nafasi hiyo ambayo hivi sasa inachezwa na Yassin Mustapha aliye katika majeraha na Adeyum Saleh.

 

Mwingine ni kipa wa Tanzania Prisons, Jeremiah Kisubi anayetajwa kusaini mkataba wa awali wa miaka miwili kwa dau la Sh 30Mil.

 

Wachezaji wote hao saba, gharama yake jumla ni Sh bilioni 1 na milioni 141.Yanga kwa kupitia Hesri hivi karibuni alifungukia usajili wa timu hiyo kwa kusema kuwa:

“Tumepanga kufanya usajili bora na wa kisasa utakaoendana na hadhi ya Yanga katika kuelekea msimu ujao.“Hakuna kitakachozuia kumsajili mchezaji yeyote tutakayemtaka ambaye yupo kwenye mipango yetu ya kumsajili kwa dau lolote lile kama ilivyokuwa kwa Mukoko na Tuisila tuliowasajili msimu uliopita.”

Stori: Wilbert Molandi | Championi

Leave A Reply