The House of Favourite Newspapers

Yanga Yatua Kwa Straika wa Morocco

0

ACHANA na Heritier Makambo, Fiston Mayele Yanga ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Wydad Casablanca ya Morocco, Francis Kazadi Kasengu, 28.


Yanga imepanga kukifanyia
maboresha kikosi chao katika safu ya ushambuliaji ambayo tayari inaripotiwa kukamilisha usajili wa Makambo aliyekuwa anaichezea Horoya AC ya nchini Guinea na Mayele wa AS Vita ya Congo.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said arejee jijini Dar es Salaam akitokea Morocco kukamilisha dili la usajili.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, safari ya Injinia kule Morocco iliishia kwa Kasengu anayeichezea klabu ya El Masry ya Misri kwa mkopo wa mwaka mmoja.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Wydad wamekubali kumuachia nyota huyo na atajiunga na Yanga mapema kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu mpya.

Alisema kuwa menejimenti ya mshambuliaji huyo imefikia muafaka mzuri na Yanga atakayesaini mkataba wa miaka miwili.

Aliongeza kuwa kiungo mshambuliaji Mtanzania, Simon Msuva anayekipiga Casablanca anahusishwa katika usajili wa mshambuliaji huyo ambaye alikuwa mwenyeji wa Injinia huko Morocco.

 

“Kama unakumbuka vizuri wikiendi iliyopita Injinia alikuwepo Morocco, alisafiri kwenda huko kwa ajili ya kukamilisha usajili wa wachezaji na kati ya hao ni mshambuliaji Kasengu ambaye yupo El Masry ya Misri akicheza kwa mkopo.

“Kutokana na ukaribu uliokuwepo hivi sasa kati ya Casablanca na Yanga wamefikia makubaliano mazuri ya kumuachia Kasengu na kumtoa El Masry alipokuwa anacheza kwa mkopo.

 


“Wamefikia muafaka mzuri
na Kasengu atakayekuja kuichezea Yanga baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili,” alisema mtoa taarifa huyo.Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Yanga, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Usajili wetu tutauweka wazi mara baada ya mchezo wetu wa mwisho wa Kombe la FA tutakaocheza dhidi ya Simba kwani tutakuwa tunakwenda ‘Pre Seasson’.”

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply