Yanga Yawaandalia Mtego Azam, Simba Benchi la Ufundi la Yanga Wafunguka Mikakati Mipya
KATIKA kuhakikisha wanapata matokeo kwenye ratiba ngumu ya michezo yao miwili ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam keshokutwa Jumatano na ule dhidi ya Simba, uongozi wa benchi la ufundi la Yanga umefunguka kuhusu kujaribu mifumo tofauti ya kiuchezaji katika safu yao ya ushambuliaji ili kutengeneza mabao mengi.
Yanga wanaoongoza msimamo wa Ligi Kuu na pointi zao 48 walizokusanya katika michezo 18, keshokutwa Jumatano wanatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Azam Complex kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji wao Azam ambao wanakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi 28.
Mara baada ya mchezo huo, kwenye Ligi Kuu Yanga wanatarajiwa kuvaana na watani zao wa jadi, Simba, katika mchezo wa dabi ya Kariakoo utakaopigwa Aprili 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatatu, kocha Msadizi wa Yanga, Cedric Kaze, alisema: “Tunakabiliwa na mchezo mgumu sana dhidi ya Azam siku ya Jumatano na baada ya hapo tutakuwa na mchezo mwingine mgumu wa Ligi Kuu mbele ya Simba lakini hili ni jambo la kawaida, tunatakiwa kuonyesha ukubwa wetu kwa kupata matokeo katika michezo hususani ile migumu.
“Hii imesababisha tuwe na utaratibu wa kujaribu mifumo tofauti hususani katika safu ya ushambuliaji kama mlivyoona kwenye michezo yetu ya kirafiki, kushambulia kwa kutumia mipira ya krosi na hata kupitia kati, hii ni katika kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu ya kushinda Ubingwa msimu huu”.
STORI: JOEL THOMAS, CHAMPIONI