The House of Favourite Newspapers

Yanga Yawasha Mitambo kwa Mkapa

0

SAFARI ya kuuanza msimu mpya wa ligi kuu Tanzania Bara imeanza jana Agosti 30, 2020 katika dimba la Benjamin Mkapa kwa Klabu ya Yanga kutambulisha wachezaji wapya pamoja na benchi la ufundi katika kilele cha Wiki ya mwananchi.

 

Sherehe hizo ziliambatana na utambulisho wa baadhi nyota wapya waliosajiliwa na klabu hiyo wakiwemo Tuisila Kisinda, Mukoko Tonombe, Michael Sarpong, Shomary Kibwana, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya, Waziri Junior  na Carlos Carlinhos.

 

Yanga ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Aigle Noir kutoka nchini Burundi ambapo mtanange huo ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2 -0.

 

Mabao ya Tuisila Kisindi katika dakika ya 39 na bao la Michael Sarpong katika ya 52 ya mchezo yalitosha kuwafanya mashabiki wa Yanga kutembea kifua mbele kwamba wana silaha nzito katika kikosi chao.

 

 

Pia katika mchezo huo iliwalazimu wageni wa mchezo huo timu ya Aigle Noir kucheza pungufu kutokana na  kadi nyekundu aliyoadhibiwa mchezaji wa timu hiyo, Koffi Kouassi, katika dakika 29 ya mchezo mara baada ya kupata kadi mbili za njano ambazo zilizaa kadi nyekundu.

 

 

Hata hivyo, kilele hicho  kilinogeshwa na burudani mbalimbali zikiwemo maonyesho tofauti kutoka kwa wasanii wa Bongo Fleva akiwemo Baba Levo, TMK Family, Chege, Shilole, Mzee Wa Bwax.

 

 

Msanii Harmonize kutoka lebo ya muziki ya Kondegang alipiga shoo ya aina yake huku akiingia uwanjani kwa staili ya kijeshi kwa kutumia kamba kutoka angani huku akikata kiu ya burudani ya maelfu ya mashabiki waliofika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

 

Hadi dakika 90 za mchezo zinaisha Yanga wanaibuka na ushindi wa bao 2-0 .

Leave A Reply