Yanga yaweka benchi Sh mil 200

Pluijm.jpg

BILA woga, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm ametamka wazi kuwa kuna ugumu kwa beki mpya raia wa Togo, Vincent Bossou kucheza kikosi cha kwanza kwani wanaocheza nafasi hiyo wanafanya vizuri.

Hapo Pluijm anamaanisha, Bossou ambaye ni chaguo lake hana nafasi ya kucheza mbele ya mabeki wa kati wa sasa wanaocheza kikosi cha kwanza ambao ni Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Bossou ambaye ametua Yanga hivi karibuni kwa usajili wa dau linalofikia thamani sawa na Sh milioni 200, amewekwa benchi katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara na kuna uhakika mdogo sana wa kucheza leo dhidi ya JKT Ruvu.

Beki huyo aliyewahi kuwa msaidizi wa kikosi cha Togo kilichokuwa chini ya nyota Emmanuel Adebayor, alisajiliwa na Yanga akitokea Goyang Hi FC ya Korea Kusini akiwa amewahi kucheza Etoile du Sahel ya Tunisia.

Plujim aliliambia Championi Jumamosi kuwa: “Bossou ni mzuri pia ni mchezaji wetu, ila kwa sasa tayari ninao Yondani na Cannavaro na wanaonyesha uwezo mzuri zaidi, wanajiamini na wanacheza kwa ushirikiano kutuletea mafanikio. Sasa hali ikiwa hivyo inakuwa ngumu kukipangua kikosi na kuingiza mwingine wakati timu imetulia na inazuia bila tatizo, lakini isieleweke kwamba Bossou hana nafasi kabisa isipokuwa tunaweza kumtumia pale inapotokea tatizo kwa Cannavaro au Yondani.”

Pluijm raia wa Uholanzi alisema anafurahishwa na uwepo wa hali ya ushindani wa nafasi katika kikosi chake kwani inamfanya kuwa na kikosi bora wakati wote.

Wakati anasajiliwa na Yanga hivi karibuni, Bossou alitegemewa kumuengua kikosini mmoja kati ya Cannavaro au Yondani lakini hali imekuwa tofauti na matarajio ya wengi akiwemo Pluijm.

JIUNGE NA MICHEZO KIGANJANI TUMA NENO SPORTS KWENDA NAMBA 15778CHAMPIONI


Loading...

Toa comment