Yawezekana Wewe Ndiye Unayesababisha Achepuke Jitathmini

 

NI Ijumaa nyingine nzuri tunapokutana katika uwanja wetu huu, kujadiliana kuhusu mambo yanayohusu uhusiano wa kimapenzi. Leo nataka tujadiliane kitu tofauti kwa lengo la kuwekana sawa. Napenda kuzungumza zaidi na wanawake. Kama wewe ni mwanamke, umewahi kujiuliza mumeo anahitaji nini zaidi kutoka kwako? Yawezekana likawa ni swali ambalo halina maana, lakini majibu yake ni mapana zaidi.

Wengi huwa wanafikiri hitaji kubwa la mwanaume kwa mwanamke, ni kufanya mapenzi, lakini je, hilo ndilo jibu sahihi? Ipo wazi kwamba tendo la ndoa ndilo linaloikamilisha ndoa, iwe imefungwa Kikristo, Kiislam, kimila au kiserikali. Hakuna ndoa ambayo inaweza kukamilika bila wanandoa kukutana kimwili, lakini je, hilo ndilo hitaji pekee linaloweza kumfanya mumeo akaridhika na wewe?

Wanawake wengi, hasa wasichana wanaoanza kuingia kwenye mapenzi, huhisi wao ni warembo, wana mvuto machoni mwa wanaume au wana maumbo mazuri, basi hiyo ndiyo tiketi ya wao kuolewa na kudumu kwenye ndoa zao. Hata hivyo, wanapoingia kwenye ndoa, wanakutana na hali tofauti kabisa kiasi cha wengine kujuta. Kinachowafanya wajute ni kwamba wameingia kwenye ndoa wakiwa hawaelewi wanaume wanahitaji nini.

 

Kwa kutofahamu huko, huelekeza nguvu nyingi kwenye tendo la ndoa, lakini mwisho hugundua kwamba kumbe tendo la ndoa siyo kitu pekee kinachoweza kuwafanya waume zao wakawapenda na kuwathamini. Hali ni tofauti kwa wanaume wasiooa ambao kwao, ipo wazi kwamba hitaji lao la kwanza kwa wanawake, huwa ni ngono na wakishakidhi haja zao, huwa hawana tena mpango. Tukubaliane kwamba mwanaume akishakuoa na kukuweka ndani, hitaji lake siyo tendo la ndoa pekee.

 

Sasa kama ni hivyo, kumbe wanaume huwa wanahitaji nini kutoka kwa wake zao? Winston Parker, ni mshauri na mtaalam wa mapenzi na uhusiano wa Marekani, katika kitabu chake cha What a Man Needs From a
Woman, anaeleza kuwa wanaume wanahitaji utiifu. Anaeleza kwamba udhaifu mkubwa wa wanaume, ni kuona wanasikilizwa, kupewa utii na kudekezwa. Hata kama mwanaume alikuwa ‘mtata’ kiasi gani, anapokutana na mwanamke anayemheshimu, kumsikiliza, kumtii na kumdekeza, ni lazima atazama kwenye penzi lake.

Ipo kasumba ya wanawake wengi siku hizi, kudai usawa hata katika mambo ambayo hayahitaji usawa. Mwanamke anakuwa jeuri, mkaidi na hamheshimu mumewe, akikatazwa kufanya jambo fulani anaona kama anatawaliwa, anafanya hata kama anajua mumewe hapendi, kisa ‘haki sawa’.

Matokeo yake, mwanaume wa aina hii akikutana na mwanamke anayemsikiliza na kumheshimu, hata kama ni hausigeli wake, yupo tayari kumkabidhi moyo wake na kumuonesha mapenzi ya dhati. Huenda hii ni miongoni mwa sababu zinazowafanya mahausigeli kupindua ndoa za mabosi.

Sihalalishi kwamba kama mwanamke ana udhaifu huu basi aadhibiwe kwa usaliti, hapana. Wengine wanakuwa na tabia hizi kwa sababu ya malezi waliyolelewa, lakini kama wakieleweshwa hubadilika. Ni matumaini yangu kwamba wanawake watakaopata nafasi ya kusoma ukurasa huu, watabadilika kwa lengo la kuzilinda ndoa zao na kujenga uhusiano imara zaidi, lakini kwa wasiotaka kubadilika, niwaambie wazi kwamba wao ndiyo sababu kubwa ya waume zao kuwa na michepuko. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

MXCLUSIVE Hashim Aziz +255 719401968 MAHABA

Loading...

Toa comment