‘Yes We Can’, Kocha Simba Atamba Waarabu Wanakufa

Kikosi cha Simba.

KWA jinsi Simba walivyopania na muziki watakaoshusha kwenye Uwanja wa Taifa jioni ya leo Mwarabu lazima alale na viatu. Ni dakika 90 dhidi JS Saoura ambazo mashabiki wote wa Simba wamehamasishana kuujaza uwanja huku wakiimba kauli mbiu yao ya ‘Yes We Can’ kuhakikisha Waalgeria wa Thomas Ulimwengu wanapigwa nyingi katika mechi hiyo ya kwanza ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa.

 

Ndani ya Uwanja John Bocco na Emmanuel Okwi wamewatoa hofu mashabiki. Golini ameomba aachiwe mwenyewe Aishi Manula. Kwenye ukuta kulia na kushoto wanasimama Gyan na Tshabalala, kati wanamaliza Wawa na Juuko Murshid. Mbabane na Nkana walilala, Saoura wanapitaje kwa mfano.

Emmanuel Okwi

Mafundi James Kotei,Jonas Mkude na Cletus Chama wanapiga shoo ya hatari kwenye kiungo. Hapo mbele hapo kuna mtu anaitwa Okwi, Meddie Kagere na John Bocco Unawazuiaje! Hebu twenzetu Taifa buana! Simba inawakilisha nchi.

 

Kampeni maalum ya ‘Yes We Can’ iliyoanzishwa na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara imepandisha mizuka ya mashabiki ambao kwenye mitaa mbalimbali wamekuwa wakihamasishana kuujaza Uwanja wa Taifa ili kuepuka fitna za Yanga ambao wamepanga kuwasapoti Saoura ambao wanavaa jezi za njano kama wao.

 

Manara amesisitiza kwamba lengo la awali ilikuwa kufuzu makundi lakini sasa ni kupata pointi 9 nyumbani na sare moja ugenini kufuzu robo fainali ili kurejesha hadhi ya kikosi hicho chenye thamani ya Sh bil 1.3.

JS Saoura

Kabla ya mechi vigogo wa Simba walijifungia sehemu na kutenga Sh mil 40 kama zawadi kwa wachezaji ikiwa timu hiyo itashinda mechi hiyo ya leo. Hata baadhi ya matawi yamechangishana fedha za motisha kwa wachezaji huku Tawi la Simba Hedikota likitoa Sh mil 10 hivyo jumla kuwa milioni 50 na zinatarajiwa kuongezeka zaidi.

 

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussem ameliambia Championi Jumamosi kuwa: “Kikubwa tunachokiangalia ni kupata ushindi kwa sababu tunacheza nyumbani.

Hatutaki kujilinda kwa kuwa tunacheza katika uwanja wetu wa nyumbani na tunachokiangalia ni matokeo ya ushindi.” “Kumkosa Nyoni (Erasto) na Kapombe (Shomari) ni tatizo lingine lakini haliwezi kutusumbua kwa sasa maana wapo watakaochukua nafasi zao japokuwa ni ngumu kidogo.

 

“Nataka kushinda mechi hii kwa kuhakikisha tunatengeneza nafasi za kutosha kwa sababu tunajua tunacheza na timu kutoka Uarabuni, tunajua vizuri tabia zao wakiwa nje na kwao lakini kwetu tunakiangalia ni kuweza kushinda.”

OKWI, BOCCO WATEMA CHECHE

Okwi na Bocco ambao wanategemewa kwenye safu ya ushambuliaji sambamba na Kagere, wamesema wamejipanga vizuri na Mwarabu lazima aumie. Wawili hao wana rekodi nzuri wanapocheza dhidi ya timu za Waarabu na wamekuwa wakifunga mabao mara kadhaa. Msimu uliopita kwenye Kombe la Shirikisho Afrika Hatua ya Mtoano, Okwi na Bocco walifanikiwa kuifungia Simba mabao mawili katika sare ya 2-2 dhidi ya Al Masry, mechi iliyochezwa Machi 7, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

 

“Tunafahamu mechi ni ngumu, lakini tumejipanga kuhakikisha tunaiongoza Simba kufanya vizuri, lengo ni kuhakikisha tunashinda mechi zote za nyumbani ili kutinga robo fainali,” alisema Okwi. Kwa upande wa Bocco, naye alisema: “Nguvu tulizozitumia kwenye hatua za mwanzo mpaka tukaingia makundi, ndizo tutakazoingia nazo katika mchezo huu wa kwanza na pengine itakuwa ni mara mbili zaidi. “Tunawaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani kutusapoti zaidi ya ilivyokuwa katika mechi ile dhidi ya Nkana ambayo tulishinda 3-1 na kufika hapa.”

 

Mwakyembe atoa onyo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, DK Harrison Mwakyembe amewaonya mashabiki wote waliopanga kwenda kuizomea Simba kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuwa na mashabiki lukuki. “Niwaonye wale ambao wamejipanga kuja kuwazomea na kuwashangilia wageni kwa sababu hilo litakuwa ni jambo la usaliti kwa nchi hivyo ni vyema wakabaki na wake zao nyumbani kwa kuangalia kwenye televisheni.” ZAWADI Bingwa Sh bil 5.2 Mshindi wa pili Sh bil 2.9 Nusu fainali Sh bil 1.8 Robo fainali Sh bil 1.5 Wa tatu kundini Sh bil 1.3 Wa mwisho Sh bil 1.3

Loading...

Toa comment