Yikpe Ajichongea, Kumpisha Tariq Yanga
UPO uwezekano mkubwa wa mshambuliaji wa Yanga, Tariq Seif kuanza kuonekana uwanjani leo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting baada ya straika raia wa Ivory Coast, Yikpe Gislain kucheza chini ya kiwango dhidi ya Lipuli FC ya Iringa.
Yikpe aliyesajiliwa na Yanga katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15, mwaka huu akichukua nafasi ya Juma Balinya aliyesitishiwa mkataba na kutua Gor Mahia ya Kenya, katika mchezo na Lipuli alishindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga mabao kabla ya kutolewa na kuingia David Molinga.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, huenda akamtumia Tariq kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu hiyo kitakachoivaa Ruvu mchezo utakaopigwa saa kumi kamili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, Tariq ni kati ya wachezaji 18 walioingia kambini kwenye Hoteli ya Regency, Mikocheni jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza tangu kocha Mbelgiji atue Jangwani.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Tariq amechaguliwa kuingia kambini kutokana na kiwango kikubwa ambacho amekionyesha kwenye mazoezi ya timu hiyo kiasi cha kumshawishi kocha ambaye alimtaka aungane na wenzake kwa ajili mchezo dhidi ya Ruvu.
Kocha huyo amefikia hatua hiyo ya kumuingiza kambini Tariq baada ya mshambuliaji wake Yikpe kukosa umakini anapofika ndani na nje ya 18 katika kufunga mabao, hivyo amempa nafasi Tariq ya kuonyesha umahiri wake wa kufunga mabao baada ya Muivory Coast huyo mwenye umbo kubwa kushindwa.
“Tangu kocha mpya Eymael ametua kuifundisha Yanga hakuwahi kumuita kambini Tariq, kwa mara ya kwanza amemchagua jana (juzi) jioni mara baada ya mazoezi ya mwisho kumalizika ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Lipuli.
“Kocha wetu mpya amekuja na mfumo mpya katika timu, siku moja kabla ya mechi timu inaingia kambini na kikosi cha wachezaji 18 pekee ambao wamekidhi vigezo kwa maana wale waliokuwa kwenye kiwango cha juu huku wengine wakirudi nyumbani.
“Lakini Tariq alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo, hivyo upo uwezekano mkubwa akawa sehemu ya wachezaji atakaowatumia katika mchezo huo, hiyo ni baada ya Yikpe kushindwa kuonyesha kiwango kikubwa katika mchezo wetu uliopita wa ligi tulipocheza na Lipuli,” alisema mtoa taarifa huyo.
Championi Jumamosi, lilikuwepo kwenye mazoezi ya Yanga yaliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Ubungo jijini Dar na kushuhudia Tariq akiongozana na wenzake kwenda kambini.





