Yondani Akubali Yaishe, Arejea Kikosini

BEKI wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani amekubali yaishe na juzi Ijumaa jioni aliingia kambini kujiunga na wenzake baada ya mgomo wake aliouweka na wenzake, Juma Abdul na Vicent Andrew ‘Dante’.

Wachezaji hao wote waligomea kambi ya timu hiyo kujiandaa na msimu mpya kwa kile kilichoelezwa kudai stahiki zao za fedha za usajili ambazo walikuwa hawajamaliziwa.

 

Nyota hao walikosa maandalizi ya msimu uliopita wakati walipokwenda kuweka kambi mkoani Morogoro kabla ya baadaye kwenda Unguja, Zanzibar.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema kuwa beki huyo ameingia kambini Ijumaa jioni wakati timu ikiwa kwenye maandalizi ya mwisho ya mchezo wa Township Rollers.

 

Hafidh alisema kuwa kurejea kwa beki huyo kutaimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo inayochezwa na Lamine Moro, Moustafa Selemani, Ally Ally na Ally Mtoni ‘Sonso’.

Aliongeza kuwa mabeki Abdul na Dante bado hawajaripoti kambini na hana taarifa za wachezaji hao ambao wameonekana kuendelea kushikilia msimamo wao.

 

“Yondani ndiye mchezaji pekee aliyeripoti kambini kati ya hao watatu wanaodaiwa kugomea kambi na ameripoti ikiwa ni siku moja kabla ya mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Township Rollers.

“Ninaamini amerejea kikosini baada ya kumalizana na viongozi wake. Hivyo upo uwezekano mkubwa wa kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Township.

 

“Hiyo ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga baada ya kusikia beki wao kipenzi Yondani akirejea kikosini na mchezo ujao atakuwepo kwenye msafara wa timu utakaokwenda kucheza na Township,” alisema Hafidh.

 

Alipotafutwa Yondani kuzungumzia hilo alikiri kurejea kikosini na kusema kuwa: “Nipo kambini tangu juzi mbona na nipo fiti kuipambania timu yangu kwenye msimu ujao.”

 

Wakati huohuo, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alikuwa mstari wa mbele kuwataka viongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti, Msindo Msolla kukamilisha malipo ya stahiki zao ili warejee kwenye kikosi kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

 

“Zahera amezungumza na wachezaji wote watatu baada ya kurejea kutoka Zanzibar, walikubali kurejea kwa sharti moja tu kulipwa stahiki zao hivyo hicho ndicho kinachofanyika kwa sasa,” alisema mtoa taarifa.

 

Akizungumzia hilo, Zahera alisema: “Nimezungumza na viongozi juu ya suala la wachezaji wote ambao wanadai stahiki zao, ninachojua hakuna mgomo ila mambo yanashughulikiwa, hivyo imani ni kwamba muda si mrefu watajiunga kikosini.”

WILBERT MOLANDI NA LUNYAMADZO MLYUKA.


Loading...

Toa comment