The House of Favourite Newspapers

Yondani Awapiga Kijembe Simba SC

0

Na Wilbert Molandi | CHAMPIONI |GPL
BEKI kisiki na tegemeo wa Yanga, Kelvin Yondani, ameitupia kijembe timu yake ya zamani ya Simba, kwa kutamka kuwa hajutii kutua Jangwani kutokana na mataji mengi ya ubingwa wanayoyachukua tangu asaini kukipiga timu hiyo.
Kauli hiyo, ameitoa mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara kumalizika dhidi ya Mbeya City iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi Jumamosi na Yanga kushinda mabao 2-1.
Kwa ushindi huo, Yanga watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulitetea taji hilo la ubingwa wa ligi kuu ambalo wamelichukua mara mbili mfululizo kabla ya msimu huu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Yondani alisema kuwa yeye ni mchezaji mwenye bahati ya kutwaa mataji ambaye tangu ametua kuichezea Yanga msimu wa 2012/2013, amebeba makombe ya ligi kuu mara tatu, Kombe la Kagame mara mbili na Ngao ya Jamii mara tatu kwa vipindi tofauti.
Yondani alisema, wakati akitwaa makombe na Yanga, timu yake ya zamani ya Simba, haijawahi kuchukua ubingwa wa ligi kuu, hivyo hajutii kusaini Yanga.
“Tangu nimeondoka Simba haijawahi kuchukua ubingwa wa ligi kuu.
“Hivyo, hata sijutii kuondoka Simba na kuja huku Yanga nikiendelea kubeba makombe ya ligi kuu na nikuhakikishie nitaendelea kubeba makombe hadi nitakapoondoka Yanga,” alisema Yondani.

Leave A Reply