The House of Favourite Newspapers

Yondani Nje, Makambo, Kaseke Ndani leo

BEKI aliyesainishwa na Yanga dakika za mwisho za usajili, Kelvin Yondani hatacheza leo dhidi ya Gormahia kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho lakini straika Mkongo, Heritier Makambo ataanza.

 

Yanga ina pointi moja tu kwenye kundi D, ikiwa imesaliwa na mechi tatu na kinachoweza kuikwamua kwenye mechi ya leo usiku ni ushindi tu wala si sare.

 

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amewaambia mashabiki wake kwamba kwenye mechi hiyo ngumu pia ataanza Deus Kaseke na Matheo Anthony na watapambana kwa kadiri ya uwezo wao.

 

Alisema kwamba Yondani kiprofeshno hawezi kumtumia kwa vile muda mwingi hakufanya mazoezi na wenzake wala hajui huko alikokuwa alikuwa kwenye hali gani hivyo atalazimika kusubiri mechi ijayo.

 

Lakini habari za ndani ambazo Spoti Xtra imezipata ni kwamba jana jioni baadhi ya viongozi wa Yanga walikuwa wakimshawishi Zahera amuanzishe Yondani kwa madai kuwa mechi ya leo ni ngumu na ana uzoefu ila kocha alisimamia misimamo yake.

 

Yanga ikitoa sare au kupoteza mchezo wa leo itakuwa ni ndoto kwao kufuzu robo fainali licha kwamba watakuwa na mechi mbili dhidi ya Rayon na USM Algiers.

 

Zahera licha ya kusisitiza kwamba watapambana lakini alionyesha wasiwasi kutokana na mwenendo wa kusuasua wa mazoezi ya wiki iliyopita kuelekea mechi hiyo ngumu ambayo Yanga alikula nne katika mechi ya kwanza nchini Kenya.

 

Kocha wa Gormahia, Dylan Kerr ameonyesha wasiwasi kutokana na maingizo mapya ya Yanga.

“Yanga tuliwafunga kule Kenya na tunapoingia kwenye mchezo huu lazima twende kwa tahadhari kubwa sababu hawawezi kukubali kupoteza tena wakiwa nyumbani.”

 

“Ila kwa upande wetu kama Gormahia tunaweza kupata kidogo taabu kwenye suala la hali ya hewa Kenya ni baridi kali na Dar ni joto hiyo itasumbua kidogo,” aliongeza Kerr.

Comments are closed.